MGOMBEA UBUNGE WA TLP KIBAMBA AMZAWADIA NG'OMBE MGOMBEA URAIS WA CCM,RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI | ZamotoHabari.

MGOMBEA wa Ubunge katika jimbo la Kibamba kupitia Chama cha 'Tanzania Labour Party (TLP),Mhandisi Aivan Maganza amemzawaidia ng'ombe mgombea wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli kutoka na utendaji wake mzuri ulioliwezesha taifa kupiga hatua kimaendeleo.

Aidha Maganza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho, amemtabiria ushindi unono Rais Magufuli katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika jumatano ya wiki hii kutokana na kukubalika na watanzania wengi.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam jana, Maganza alisema kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa TLP Augustino Mrema aliyemkabidhi Rais Magufuli zawadi ya mbuzi, yeye pia ameguswa na utendaji wa Kiongozi huyo.

"Tayari zawadi ya Ng'ombe huyo ipo Dodoma ambapo ni nyumbani kwetu, namsubiri amalize ratiba zake za kampeni ili niweze kumkabidhi kama shukrani na pongezi kwa alicholifanyia Taifa hili" alisema Maganza.

Alisema utendaji wa Kiongozi huyo mkuu wa taifa hili haufananishwi kwa vyovyote na  wengine kutokana na mambo mengi mazuri aliyoyafanya katika taifa hili ndani ya kipindi cha miaka mitano cha awamu yake ya kwanza madarakani.

Pamoja na hilo Maganza pia alisema kitendo cha Rais Magufuli kuliwezesha taifa kufikia uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa, kinazidi kupaisha sifa zake katika utendaji, jambo lililowafanya watanzania wengi kujenga imani naye.

Aidha akizungumzia mwenendo wa jimbo lake katika mchakato huu wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika keshokutwa, Maganza alisema ana imani kuwa atashinda kiti hicho kutokana na mikakati yake mizuri aliyoitoa kwa wananchi hao.

" Ukweli kwa sasa wananchi wanasubiri siku ya keshokutwa ili kufanya maamuzi ila kitu kitu kipo sawa hadi hivi sasa, nina imani kubwa kuwa wananchi wa jimbo langu la Kibamba hawatoniangusha" alisema Maganza.

Aidha aliwaomba wananchi kujitokeza kwa weingi na kutumia nafasi yao ya kikatiba kupiga kura na kuwachagua viongozi mbalimbali kwa kuwa hiyo ndiyo fursa pekee ya wao kupata maendeleo.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini