Charles James, Michuzi TV
ASUBUHI ya Oktoba 8, 2015 Ndege ndogo ya kukodi inatua katika uwanja wa Kimataifa wa John Lennon, jijini Liverpool. Anashuka jamaa mrefu akiwa amevalia Jeans ya blue, shati jeusi na koti la suti jeusi, usoni akiwa na mawani yake.
Anapokelewa na Maboss wa Klabu ya Liverpool, Mwenyekiti Timo Werner na Mike Gordon ambaye ni Rais wa FSG ambayo ni wamiliki wa Klabu hiyo.
Ni Jurgen Klopp ndiye alikua amepokelewa akitokea nchini Ujerumani tayari kuja kusaini mkataba wa kumfanya kuwa Boss mpya wa benchi la ufundi la Liverpool baada ya kufukuzwa kwa Brendan Rodgers.
Werner na Gordon wanamchukua hadi Anfield, anatembezwa kwenye kila korido, ofisi na viunga vyote. Kisha wanamuingiza ndani ya uwanja wa Anfield.
Anaoneshwa jukwaa la Spion Kop kaskazini mwa uwanja wanapokaa mashabiki wafia timu wa Liverpool, anaoneshwa jukwaa la Kop End na mengine.
Kama haitoshi wanampeleka ilipo makumbusho ya mataji pale Anfield. Wanamuonesha rekodi kubwa ya makombe.
Cha ajabu rekodi inasoma mara ya mwisho kubeba Kombe la Ligi Kuu ni msimu wa 1989/90. Mara ya mwisho kubeba kikombe chochote ni mwaka 2012 tulivyobeba taji la Capital One siku hizi linaitwa Carabao.
Mara ya mwisho kubeba Ligi ni miaka takribani 30 iliyopita. Klopp anavua miwani yake anaifuta na kuivaa tena. Miaka 30 bila Ligi? Hii maana yake yeye ameletwa kuja kurudisha heshima iliyokwisha potea. Mbona kazi ngumu hii?
Kisha wanamtoa hadi nje ya uwanja kwenye lango kuu ilipo sanamu ya Baba wa Liverpool, Bill Shankly. Wanamwambia heshima yako itamfikia huyu mzee endapo utatupa ubingwa wa Ligi.
Baada ya hapo wanaelekea kwenye mkutano na wandishi wa habari. Na hapo ndipo Klopp alipozindua tumaini jipya kwa wana Liverpool duniani. Maneno yake yalikua tiba tosha.
Akijibu swali la James Pearce; Klopp anasema " It is not a normal club, it is a Huge Club, we have to change from doubters to believers"
Tafsiri isiyo rasmi anasema "Hii siyo klabu ya kawaida, ni klabu kubwa, ni lazima tubadili mawazo yetu kutoka wasioamini kuwa wanaoamini,"
Akaongeza kuwa hawezi kuahidi ubingwa kwa haraka lakini ndani ya miaka minne asipoipa ubingwa wowote basi ataachana na Liverpool na kwenda kufundisha soka nchini Uswis. Maneno ya kijasiri haya.
Ni baada ya hapo tukashuhudia kuanza kutokea kwa mabadiliko kwenye timu hiyo taratibu taratibu, ile roho ya kipambanaji ya ki-Liverpool ikaanza kurejea.
Klopp akajenga imani kubwa ya mashabiki na viongozi kwake, akabadilisha mioyo ya wachezaji kujua na kutambua thamani ya jezi ya Liverpool, akamuaminisha Jordan Henderson ni bora kuliko Xavi, Mammo Sakho ni bora kuliko Ramos na Dani Sturridge ni levo za Leo Messi.
Timu ikabadilika, moyo wa kuifia Timu ukaanza kuonekana, watu wakaicheka Liverpool iliposhangilia sare dhidi ya West From Disemba 2015 baada ya Origi kusawazisha dakika ya 96.
Klopp anasema baada ya mechi ile ndio Liverpool mpya ilizaliwa, kitendo cha kupambana hadi dakika ya 96 kutafuta matokeo kwenye uwanja wetu wa nyumbani kilijenga imani kwa mashabiki.
MIAKA MITANO NA KLOPP HAJAENDA USWISI
Ametimiza ahadi yake ya makombe pale Liverpool, miaka mitano aliyoitimiza leo imetosha kumfanya kuwa miongoni mwa makocha sita wanaoheshimika zaidi kwenye viunga vya Melwood.
Pengine baada ya Shankly na Bob Paisley ni Klopp anaefuata, na labda angekua muingereza heshima ingekuwa kubwa zaidi.
Ni Klopp aliekuja na kuikuta Liverpool haijiwezi hata kucheza na timu za daraja la kwanza kwenye michuano ya FA na kombe la Ligi.
Walikua wabovu kila eneo, hata uwezo wa kusajili wachezaji wakubwa haukuepo, kipindi flani Karim Benzema alisema Liverpool siyo timu ya hadhi yake. Eti ni wadogo kuliko yeye.
Christian Eriksen, Mousa Dembele na Clint Dempsey waliwakataa wakaenda Spurs, Sitosahau Willian alivyoifungia vioo na kusaini Chelsea.
Nani angekuja kwenye Timu inayomaliza msimu ikiwa nafasi ya nane? Hawachezi Ligi ya Mabingwa wala Europa League. Walikua 'unga' kila idara.
Oktoba 8 inabaki kuwa ya heshima kwao, Klopp amewafanya leo kuzungumzwa kuliko timu yoyote duniani. Juzi Man U walifungwa sita wao wakafungwa saba stori iliyopo duniani ni Liverpool kupigwa saba siyo kichapo cha United.
Maana yake Liverpool ndio Timu inayoogopwa kuliko wengine, wanatishia amani za Timu zao, wamekua imara kwenye Ligi hadi kwenye michuano ya Ulaya.
Tazama tuna misimu mitatu hawajawahi kufungwa mchezo wa Ligi kwenye uwanja wao wa nyumbani (Anfield), msimu wa tatu huu unaanza wamefungwa mechi nne tu kwenye Ligi.
Misimu mitano wana makombe manne makubwa duniani, Ligi Kuu, Super Cup, Uefa Champions league na Kombe la Dunia ngazi ya Klabu. Hii yote ni sababu ya Klopp.
Amewatengeza kuwa timu tishio isiyokubali kukata tamaa toka walivyodroo siku ile na West Brom. Ametufanya kuwa timu inayotamaniwa na wachezaji wengi bora duniani kwa sasa.
Miaka mitano ya Klopp wamekua wababe hadi kwenye soko la usajili, fikiria Virgil Van Djik aliigomea Man City, Chelsea ili aje Anfield, Fabinho aliikacha Man United akaja Liverpool. Usisahau sajili za Naby Keita na Allison Becker pia.
Juzi tu tumeona Thiago Alcantara amegoma kusaini mkataba mpya Bayern Munich tu kwa sababu anataka kwenda Anfield. Lile kumbatio la Klopp limewafuta Liverpool machozi.
Na sasa msimu uliopita wamekata kiu yao ya muda mrefu, njaa ya miaka 30 bila ubingwa imeisha, sasa wanaitwa mabingwa wa EPL, wapi wangepata hii heshima bila Klopp?
Msimu huu amesema haendi kutetea taji lake la EPL Bali anaenda kulipigania, goli saba walizofungwa na Villa haziondoi ukweli kwamba wanaenda kubeba tena hii Ligi kwa mara ya pili mfululizo na wapinzani wanalijua hilo.
Alisema asipobeba Kombe kwa miaka mitatu ijayo ataenda kufundisha soka Uswisi, miaka mitano leo yupo bado Anfield na hakuna ambaye anataka aondoke.
Mashabiki wa Liverpool wanasema hata akifa leo waraendelea kulilipa kaburi lake mshahara. Miaka 30 ya kutokwa machozi, kutukanwa, kudhalilishwa imemalizwa na Klopp.
Kama usemavyo wimbo wao wa Klabu wa You'll Never Walk Alone, " At the end of the storm there is a golden,".
0683 015145
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments