Na Muhidin Amri,
Tunduru
WAKAZI wa kijiji cha Milonde kata ya Matemanga wilayani Tunduru, wameishukuru serikali kwa kukamilisha mradi mkubwa wa maji ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2012 ambao umesaidia kumaliza kero ya muda mrefu ya maji safi na salama.
Habibi Kassim na Rehema Awadhi wamesema, hapo awali walilazimika kuamka kati ya saa 10 na 11 alfajiri kwenda kutafuta maji katika vyanzo visivyo rasmi huku wakati mwingine wakikutana na wanyama wakali wakiwemo Tembo na Nguruwe pori.
Asema,kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao kwa sababu mbali na kumaliza kero ya muda mrefu pia utachochea maendeleo ya wananchi wa kijiji hicho na kata mzima ya Matemanga.
Naye Rehema Awadhi ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Milonde alisema, siku za nyuma walilazimika kwenda shule wakiwa wachafu kutokana na kukosekana kwa maji ambapo ameishukuru serikali kukamilisha mradi wa maji Milonde.
Hata hivyo,ameiomba wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa)kuongeza vituo vya kuchotea maji katika hicho ili kupunguza kero kwa watu kutumia muda mrefu kwenye vituo vilivyopo kwa ajili ya kupata huduma ya maji.
Alisema, licha ya serikali kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ulioanza kujengwa miaka 12 iliyopita,hata hivyo bado kuna changamoto ya wananchi kukaa muda mrefu katika vituo vya kuchotea maji.
Amesema, vituo saba vilivyopo havitoshi jambo linalo sababisha watu kukaa kwa muda mrefu na wakati mwingine kutokea kwa vurugu ya kugombea maji na hata kupoteza muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Ameongeza kuwa,ipo haja kwa Ruwasa kuhakikisha vituo vya kuchotea maji vinaongezwa kwani katika kijiji hicho kuna idadi kubwa ya watu ikilinganisha na vituo vilivyojengwa.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa maji vijijini na mijini(Ruwasa)wilaya ya Tunduru Primy Damas alisema, vituo vilivyojengwa kwa ajili ya kuchotea maji katika kijiji cha Milonde ni 12 ambapo kwa sasa vinavyofanya kazi ni 7.
Kwa mujibu wake,hali hiyo imetokana na kushindwa kupata kibali cha kupitisha mabomba kutoka kwenye tanki kwenda katika vituo vya kuchotea maji kutoka kwa wakala wa barabara Tanroad, kwani miundombinu ya mradi huo ni lazima ipite katikati ya barabara .
Aidha alisema, mradi wa maji Milonde umetengewa kiasi cha shilingi milioni 215,212,257.13 na hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 72,388,633.64 ambapo mradi huo umekusudia kuhudumia wananchi zaidi ya 3,000.
Alisema, mradi huo umegharamiwa na Serikali kuu kupitia wizara ya maji na kutekelezwa ma Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Tunduru kwa kutumia njia ya force Account ambapo pia wananchi wanachangia nguvu zao kwa kushiriki shughuli za ujenzi.
Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa wizara ya maji Dkt Christopher Nditi katikati akimsikiliza meneja wa wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru Primy Damas wa kwanza kulia kuhusu ujenzi wa mradi wa maji Milonde kata ya Matemanga ambao umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 3000 wa vijiji vinne vya Milonde,Matemanga,Jaribuni na Changarawe kwa gharama ya zaidi ya milioni 111.
Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa wizara ya maji Dkt Christopher Nditi wa pili kulia akishuhudia mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Milonde wilayani Tunduru Rehema Awadhi akichota maji katika moja ya kituo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji Milonde ambao ulianza kutekelezwa miaka 12 iliyopita,katikati meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Primy Damas na wa kwanza kulia mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Habibi Kassim.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments