Yassir Simba, Michuzi TV
Muendelezo wa ligi kuu Tanzania bara VPL umeendelea tena Oktoba 26 ,2020 katika dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo klabu ya Simba iliwakaribisha Ruvu Shooting kutoka Mlandizi Mkoani Pwani huku Simba wakipoteza mchezo wao wa pili mfululizo katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu 2020/2021 kwa kuadhibiwa na Ruvu Shooting bao moja kwa sifuri.
Mchezo huo uliopigwa majira ya saa kumi kamili jioni umeshuhudia klabu ya Ruvu Shooting ikifuta uteja dhidi ya Simba ambapo wamepata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mnyama ambapo makosa yaliyofanywa na mlinzi wa klabu ya Simba Pascal Wawa katika harakati za kuokoa mpira katika eneo la kumi na nane la Simba ulimkuta Fully Zulu Maganga mshambuliaji hatari wa Ruvu Shooting na kuipatia klabu yake bao la kuongoza na la ushindi katika mchezo mnamo dakika thelathini na sita ya mchezo katika kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba wakilisakama lango la Ruvu Shooting kwa mashambulizi makali huku nao Ruvu wakijilinda kwa ustadi zaidi wakiongozwa na beki Mkongwe na mzoefu wa klabu hiyo Juma Saidi Nyosso huku Simba wakipata mkwaju wa penati mnamo dakika ya sabini na moja ya mchezo mara baada ya mlinzi wa Ruvu Shooting kumtendea madhambi mshambuliaji wa timu ya Simba Luis Miquissone ambapo muamuzi wa mchezo huo aliamuru mkwaju wa penati upigwe katika lango la Ruvu Shooting , penati hiyo iliopigwa na mshambuliaji wa Simba John Rafael Bocco iligonga mwamba na kushindwa kutinga wavuni.
Licha ya klabu ya Simba kupata penati katika mchezo huo, kulikuwepo na vurugu za hapa na pale mara baada ya wachezaji wa Ruvu Shooting kutoridhishwa na maamuzi yaliotolewa na muamuzi wa mchezo hali iliyopelekea mchezaji wa Ruvu Shabani Msala kupewa adhabu ya kadi nyekundu katika dakika ya themanini ya mchezo hali iliyopelekea Ruvu Shooting kucheza pungufu katika muda uliyosalia.
Rasmi Simba anashuka hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu akivuna alama kumi na tatu katika michezo saba huku Ruvu Shooting wao wakishika nafasi ya saba wakiwa na alama kumi na mbili walizovuna katika michezo nane ya ligi kuu Tanzania bara huku licha ya klabu ya Azam kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar Jamhuri mkoani Morogoro bado wanasalia kuwa vinara wa katika msimamo wa ligi wakicheza michezo nane wakipata alama ishirini na moja.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments