KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI AMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI KWENYE JIMBO LA NDUGA | ZamotoHabari.

TUNATEKELEZA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kumaliza changamoto ya Maji katika vijiji vya Ndurugumi na Suguta wilayani Kongwa, Dodoma ambapo kiasi cha Sh Milioni 400 zinapelekwa wiki hii kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miradi miwili ya maji itakayomaliza changamoto hiyo kwenye vijiji hivyo viwili na vilivyo jirani.

Hayo yametokea katika ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ambaye aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenda kuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo ambao kwa muda mrefu wamekua wakiangaika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Akizungumza katika vijiji hivyo Mhandisi Sanga amesema serikali ya awamu ya tano kupitia wizara ya maji haina maneno mengi bali vitendo hivyo fedha hizo zitaletwa ndani ya wiki hii kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miradi hiyo huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati wa kuchimba mitaro.

" Hapa Ndurugumi nilishatuma watafiti wangu wakaniambia inahitajika Milioni 910 ili mpate maji sasa tutawaletea hiyo hela na wiki hii Milioni 200 zitatangulia na ndani ya siku 14 kazi ya kujenga tanki la lita laki tatu ianze mara moja na ndani ya siku 90 watu wa Ndurugumi na vijiji jirani waanze kunywa maji hapa.

Kijiji cha Suguta nimeona changamoto yenu, nafahamu hapa panahitajika Sh Milioni 510 ili muweze kunywa maji niwaahidi wiki hii serikali yenu inaleta Sh Milioni 200 za kuanzia na ninaagiza kazi ianze ndani ya siku saba na ndani ya siku 60 ukamilike,hizi na kiasi kingine kilichobaki tutakitoa Januari na Februari, tunachotaka ni watu wa Kongwa wanufaike na matunda ya Serikali yao," Amesema Mhandisi Sanga.

Amewataka wananchi wa vijiji hivyo na maeneo mengine yenye miradi ya maji kuitunza miradi hiyo kwa wivu mkubwa kwani fedha zilizotumika zimetokana na kodi za watanzania huku akiwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuchangia kiasi kidogo pale itakapohitajika.

Kwa upande wake Spika Ndugai amemshukuru Katibu Mkuu Sanga kwa kuwa msikivu na kwenda kujionea kero wanazokumbana wananchi wake huku akimuahidi kwamba watalinda miradi hiyo kwa nguvu zote na kwamba wapo tayari kushiriki ujenzi huo pindi utakapoanza.

" Tunashukuru sana Mhandisi Sanga, wewe ni Mtendaji na umethibitisha hilo hapa, changamoto ya maji tuliahidi wakati wa kampeni kwamba tutaitatua na leo tuna furaha kuona kweli tumeanza kuitatua, nikuombe usichoke kuja Kongwa," Amesema Spika Ndugai.

Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Ndurugumi wilayani Kongwa katika ziara ya kutatua changamoto ya maji. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dk Selemani Serera.
Moja kati ya miradi ya maji inayotekelezwa katika Wilaya ya Kongwa ukiwa kwenye hatua za mwisho kukamilika. Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ameagiza ukamilike kwa wakati.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza katika mkutano wa kutatua changamoto ya maji kijiji cha Suguta wilayani Kongwa. Kulia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Selemani Serera akizungumza katika mkutano wa kutatua changamoto wa maji katika kijiji cha Suguta.
Wananchi wa Kijiji cha Suguta wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipofika kuzungumza nao na kusikiliza changamoto za Maji zinazowakabili.
 

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini