TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA YAENDESHA MAFUNZO YA KITAIFA YA USALAMA WA MIONZI KWA WATAALAM 73 WA MIONZI | ZamotoHabari.

Jumla ya wataalam 73 wanaotoa huduma katika vyanzo vya mionzi kwa ajili ya uchunguzi na tiba kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini wanashiriki katika mafunzo ya Kitaifa ya Usalama wa Mionzi yanayoendeshwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) jijini Arusha.

Mafunzo haya yaliyoanza jana Jumatatu tarehe 14 Novemba 2020 yatafanyika kwa muda wa siku tano, mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo yaliyofanyika mwaka jana 2019.

Akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Mionzi wa TAEC, Dkt. Justine Ngaile amewataka washiriki hao kuhakikisha wanapata uelewa mzuri katika mafunzo hayo utakaowasaidia katika kuhakikisha wanalinda afya za watanzania ili wasipate madhara yatokanayo na mionzi.

Dk. Ngaile amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea washiriki ufahamu juu ya matumizi salama ya mionzi na jinsi ya kujikinga na madhara ya mionzi, pia kutambua viwango vya mionzi ambavyo ni salama kwa wafanyakazi katika maeneo ya kazi ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na mionzi, hii ni pamoja na kufuata sheria za usalama wa mionzi mahala pa kazi bila kusahau kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa inayoelekeza namna salama ya matumizi ya mionzi.

“Mtajifunza kwa kina masuala ya usalama wa mionzi katika maeneo ya kazi, kwani usalama wa mionzi ni nyenzo muhimu katika kulinda wagonjwa, wafanyakazi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi. Hivyo basi, naamini mtajengewa uwezo mkubwa na watalaamu wa TAEC” alisema Dkt. Ngaile.

Dkt. Ngaile aliwahakikishia washiriki kwamba TAEC itaendelea kutoa mafunzo ya namna hii katika kuhakikisha inawalinda watanzania dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati vyanzo vya mionzi vinapotumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani, katika migodi, kwenye ujenzi, maeneo ya utafiti na katika vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma kwa kutumia mionzi hapa nchini.



 

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini