Mbunge Kamonga akoshwa na ukusanyaji mapato Ludewa | ZamotoHabari.

Na Amiri Kilagalila

MBUNGE wa Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe Joseph Kamonga amewaomba madiwani  kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri hiyo ili kufikia malengo ya kuwakomboa wananchi kiuchumi katika kuboresha sekta ya afya,elimu na miundombinu

Kamonga ameomba hayo mara baada ya hafla ya kuwaapisha madiwani iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya na kuongeza kuwa wasisubiri serikali itumie nguvu katika kufanikisha hilo. 

“Wakuu wa Idara mimi ni mtaalamu mwenzenu nimekuwa kwenye utumishi wa halmashauri kwa muda mrefu,ninaomba tushirikiane katika ukusanyanyi wa mapato” alisema Kamonga

Aliongeza “Tusipohangaika kukusanya mapato,tutashindwa kutatua changamoto za wananchi,tuendelee kuhamasishana tukiamini jukumu la kuleta maendeleo ni letu sote” alisema Joseph Kamonga

Aidha amempongeza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwa kuendelea kukuza kiwango cha ukusanyaji wa mapato.

“Mwaka wa kwanza aliofika mkurugenzi alikusanya milioni 600 ,mwaka uliofuata alikusanya milioni 800 na mwaka huu amesema ana mpango wa kukusanya zaidi ya bilioni moja na mpaka sasa ameshafikisha 55%”alisema Kamonga

Vile vile amesema katika swala la usafiri kwenye ziwa nyasa kutokana na kusimamishwa ataendelea kufuatilia ili kujua zaidi kuhusu usafiri huo “Kule ziwa Nyasa tunashukuru Rais alitutengenezea meli tatu lakini meli zile zilifanya safari moja halafu zikapaki,tunaendelea kufuatilia kuhakikisha wananchi waliotuchagua hatuwaangushi” Wakili Joseph Kamonga

 

Aidha, kwa upande wa katibu tawala wa wilaya ya Ludewa, Zaina Mlawa amewataka madiwani wote kuhakikisha kuwa mpaka kufikia Januari 30, 2020 watoto waliofaulu darasa la saba na kupangiwa shule wanaripoti katika shule walizopangiwa na kuanza masomo.

 

Amesema, mara nyingi idadi ya wanafunzi waliofaulu na kupangiwa shule ni tofauti na idadi ya wanafunzi wanaripoti katika shule hizo kitu ambacho kinashusha ukuaji wa sekta ya elimu katika wilaya hiyo.

 

"Madiwa mkisimama vyema katika nafasi zenu mnaweza kuleta maendeleo ya elimu katika kata zenu na wilaya kwa ujumla, hivyo mhakikishe mnatekeleza hili kwa ushirikiano na wazazi,"amesema Mlawa.

 

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya uapisho wa madiwani hao,amewaomba madiwani kuhakikisha wanawekwanda kusimamia miradi ya maendeleo kikamilfu kwa kuwa serikali imejitahidi katika sekta mbali mbali ikiwemo afya elimu,nishati na maji.

 

“Kwa hiyo madiwani bado mnayo nafasi kubwa kuhakikisha yale ambayo serikali haijayakamilisha sasa tunakwenda kuyakamilisha kwa kuwa wananchi wanamatarajio makubwa na serikali yao”alisema Rubirya

 

Willbard Mwinuka ni mmoja wa madiwani walioapishwa katika baraza hilo,amesema kuwa wameyapokea yote waliyoaswa na wakuu wa idara mbalimbali pamoja na mbunge na wataenda kutekeleza kwa kila hali ili kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.

 

Amesema kwa upande wake amejipanga vyema katika kufanya kazi kwa bidii na atahakikisha analeta maendeleo katika kata yake na wilaya kwa ujumla.

Wakili Joseph Kamonga mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Baadhi ya madiwani wakiwa makini kusikiliza hotuba ya mkuu wa mkoa wa Njombe alipofika katika kikao hicho cha baraza la madiwani

Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa rubirya akizungumza na madiwani.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini