Takukuru yamrejeshea Sh5.48 milioni mwalimu anayedai kutapeliwa na Qnet | ZamotoHabari.

 


Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita imemrejeshea Sh5.48 milioni Rose Mgomba anayefundisha Shule ya Msingi Lukaranga aliyedai kutapeliwa na kampuni ya Qnet.


Akizungumza na gazeti hili, mkuu wa Takukuru mkoani humo, Leonidas Felix alisema walipata malalamiko kutoka kwa mwalimu huyo na walipofanya uchunguzi waligundua kuwa Qnet imemdhulumu kwa njia za ushawishi, kurubuni na kuahidiwa kutengeneza faida ya fedha maradufu baada ya kuwezeshwa kufungua akaunti ya ununuzi wa bidhaa za kampuni hiyo mtandaoni.


Wasiwasi watanda kampuni ya Qnet


“Tumebaini kuna kampuni inayojulikana kwa jina la Qnet inayojihusisha na biashara ya mtandaoni. Kampuni hii imelalamikiwa na Rose Mgimba wa mjini Geita baada ya kudhulumiwa kiasi cha Sh5.48 milioni.”


“Baada ya uchunguzi dhidi ya malalamiko hayo imebainika kuwa kampuni hiyo ya Qnet inaendesha biashara hiyo kwa kuwatumia watu wanajiita wawakilishi huru ambao ndio wanaowashawishi na kuwalaghai watu kujiunga katika mtandao wa biashara hii,” alisema.


Ofisa Halmashauri mbaroni kwa tuhuma za kutapeli watumishi wa umma


Katika uchunguzi wao, alisema walibaini kampuni hiyo haijasajiliwa na msajili wa makampuni kufanya biashara na haina leseni ya biashara nchini.


“Kibaya zaidi kinara na kiongozi wa wawakilishi huru hawa mkoani Geita aitwaye (anamtaja) anafanya biashara hiyo kupitia mwamvuli wa taasisi yake isiyokuwa ya kiserikali (NGO) (anaitaja),” alisema.


Pia alisema miongoni mwa wawakilishi huru ni watumishi wa umma waliojiunga na mtandao huo ambao wanatumika kuwashawishi watumishi wenzao kujiunga huko wakijua ni mtandao wa biashara haramu ambao ili uendelee kukua unatakiwa kuendelea kusajili wana mtandao wengi zaidi.


“Kwakuwa mwalimu Rose Mgomba alilalamika Takukuru, umefanyika uchunguzi ukabaini kweli amedhulumiwa kiasi cha Sh5.48 milioni kwa ahadi ya kufunguliwa duka mtandaoni na mwisho wa siku aliletewa bidhaa ambazo aliambiwa ni kwa matumizi yake ya nyumbani na siyo dukani na kwamba aendelee kushawishi wateja wengine wajiunge.”


“Kwakuwa wahusika walibanwa wakarejesha fedha hizo walizomdhulumu huyu mwalimu leo anakabidhiwa fedha zake zote Sh5.48 milioni,” alisema mkuu huyo wa Takukuru mkoani Geita.


Aliwataka Watanzania na watumishi wa umma hasa walimu wajiepushe kujiunga na biashara wasizokuwa na uhakika nazo wakikumbuka kwamba hakuna njia ya mkato kujiingizia kipato kikubwa bila kufanya kazi ili kujiepusha na uharifu wa namna yoyote ikiwemo ukwepaji kodi, uhujumu uchumi na utakatatishaji fedha.


“Kwa kuwa biashara hii inafanyika kwa njia haramu, Takukuru kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama tutaendelea kuwasaka wana mtandao wote mkoani Geita ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na hatutaruhusu biashara hii kuendelea mkoani hapa na wananchi wetu kuendelea kudhulumiwa,” alisema.


Katika hatua nyingine kamanda Felix alisema wamekamata masanduku 19 ya viuwatilifu aina ya duduba EC450 vilivyokuwa vimetolewa na Bodi ya Pamba kwa ruzuku ya Serikali kwa ajili ya wakulima wa Chama cha Ushirika (Amcos)cha Bukanga kinachojumuisha vijiji viwili vya Bulela na Gamashi mkoani humo.


Viuatilifu hivyo alisema vilikuwa vimechepushwa na mhasibu wa chama hicho ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini