Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwahutubia wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa OSHA wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza la baraza hilo la nne.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza la baraza hilo la nne.
Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa OSHA wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha baraza la nne la wafanyakazi wa OSHA.
Na Mwandishi, Morogoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, amesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni Taasisi yenye nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa agenda za kitaifa na kimataifa ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Kwanza cha Baraza la Nne la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika Mkoani Morogoro.
Waziri Mhagama amesema shughuli zote za kiuchumi ambazo zimeipelekea nchi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ikiwemo uzalishaji kupitia viwanda zinahitaji mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kupelekea ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Katika kila eneo la kazi linaloanzishwa kunakuwa na vihatarishi mbali mbali vinavyoweza kuleta athari kwa wafanyakazi katika eneo husika hivyo pasipokuwa na chombo madhubuti cha kusimamia na kutoa miongozo ya kuwakinga wafanyakazi hakuna shaka kwamba Taifa linaweza kupoteza nguvu kazi yake kutokana na wafanyakazi kuumia au kupata magonjwa yatokanayo na kazi na hivyo kupelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la wategemezi,” alisema Waziri Mhagama.
Mhagama ameiagiza Taasisi ya OSHA kuendelea kuboresha mifumo ya kiutendaji ili kuiwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kutenga muda mahususi wa kusikiliza na kutatua kero mbali mbali za wadau kote nchini.
Aidha, Waziri Mhagama amewataka watumishi wa OSHA katika baraza hilo kufanya kazi kwa bidii, kujiepusha na vitendo rushwa na kuwa wazalendo kwa nchi yao ili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Akimkaribisha Waziri ambae alikuwa Mgeni Rasmi katika kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema kwasasa Taasisi yake inafanya vizuri kiutendaji jambo ambalo limepelekea Taasisi hiyo kuvuka malengo yake kiutendaji katika mwaka wa fedha uliopita (2019/2020).
“Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Juni 2020, OSHA ilifanikiwa kusajili sehemu za kazi 6,837 ukilinganisha na lengo la kusajili maeneo ya kazi 5,306 na kukagua maeneo ya kazi 16,923 ambayo yalifanyiwa jumla ya kaguzi 173,116,” alisema Mkuu huyo wa Taasisi.
Kwa mujibu wa Taarifa aliyoitoa Mwenda kwa Waziri, ukaguzi huo ulijumuisha ukaguzi wa; Usalama wa umeme, mitambo ya kuzalishia mvuke (Steam Boilers), Mitungi ya gesi na hewa (Air Receivers), Majengo na Majenzi, Egonomia, Zana za Kunyanyulia vitu vizito (Lifting Appliances) pamoja na Vipimo vya ubora wa mazingira ya kazi.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sarah Rwezaura, ameupongeza uongozi wa OSHA kwa kuzingatia kanuni za utawala bora na kuwashirikisha wafanyakazi katika kufanya maamuzi muhimu yanayohusu Taasisi yao kupitia vikao vya baraza la wafanyakazi.
Mwakilishi wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Serikalini, Fidelis Gakuba, amewakumbusha wajumbe wa baraza hilo kuwa wao ni sehemu ya serikali na endapo hawatatekeleza wajibu wao ipasavyo watapelekea ongezeko la malalamiko dhidi ya serikali.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments