Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameiagiza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kuongeza ubunifu katika kutoa huduma na kujiendesha kibiashara ili iendane na soko la ushindani.
Waziri Bashungwa amesema hayo Desemba 14, 2020 alipotembelea Kampuni hiyo Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwamba magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo ni kioo katika kuelimisha umma kwa kuzingatia uzalendo, hivyo ni nyema yakaongeza kasi zaidi.
“Nawapongeza mnafanya kazi nzuri, lakini nasisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuandaa na kuchakata habari zenye usahihi na ukweli zitakazosaidia jamii, tumieni lugha fasaha ya Kiswahili kwa yale magazeti ya Kiswahili, na endeleeni kuongeza ubunifu kama ambavyo mmeanza kufundisha kupitia magazeti lugha yetu ya Kiswahili”,alisema Mhe.Bashungwa.
Mhe Bashungwa ameongeza kuwa atashirikiana na TAMISEMI kuona namna ya kutumia Kampuni hiyo katika kuchapisha madaftari ya wanafunzi kwakua Kampuni hiyo ina uwezo wa kufanya hivyo, huku akiongeza kuwa taasisi za serikali zinatakiwa kutumia Kampuni hiyo katika kuchapisha maandiko, majarida, vipeperushi na machapisho mbalimbali.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdalaah Ulega ameitaka kampuni hiyo kuona namna ya kuwekeza katika dijitali hasa katika kuweka maudhui ya michezo na Sanaa ambayo yana watazamaji na wasomaji wengi lakini pia itasaidia kuongeza mapato.
“Hongereni kwa kazi nzuri, magazeti yanayozaliswa hapa ni makongwe katika kuhabarisha umma na yanahitaji kufanyiwa mabadiliko ili yaendane na uhitaji wa wateja”,alisema Mhe.Ulega.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Kampuni hiyo imeendelea kufanyiwa maboresho ambapo watumishi wenye sifa tayari wameingizwa katika mfumo wa mshahara wa serikali.
Naye Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo Bibi. Tuma Abdallah amesema miongoni mwa mafanikio ambayo kampuni imepata ni kuanzisha Jukwaa la Biashara ambalo linatoa fursa kwa wafanyabiashara kutangaza biashara zao, huku akieleza kuwa Kampuni hiyo imedumu sokoni kwa takribani miaka 90 ambayo imepitia vipindi tofauti vya mabadiliko.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments