Kuokotoze ramani na kisha kuijenga ni kutokuthamini kile unachokwenda kujenga licha ya kwamba unatumia mamilioni ya pesa kujenga. Inashangaza sana kwamba unakuta mtu anaenda kujenga nyumba ya milioni 90 lakini naokoteza ramani au anatafuta ramani ambayo imetumiwa na mtu mwingine wakati gharama ya kutumia mtaalamu kwa huduma yote ya ushauri pamoja na michoro labda ni 600,000/= ambayo haifiki hata 1% ya gharama yote ya ujenzi. Maamuzi ya aina hii ni maamuzi ambayo kwa vyovyote vile yanaambatana na hasara kubwa.
Madhara ya kuokoteza na kupata ramani ya nyumba kisha ukaijenga.
Iwe ni kutoka kwenye mitandao, au ni kutoka kwa mafundi wa mitaani au kwa namna nyingine yoyote ile, kuokoteza ramani na kisha kuijenga ni kushindwa kuuthamini mradi unaotaka kuujenga licha ya kwamba unakwenda kutumia pesa nyingi sana kuujenga, na madhara yake ni kama ifuatavyo.
-Utashindwa kupata unachotaka: Unapookoteza ramani maana yake ni kwamba unalazimika kukubaliana na chochote kilichoko kwenye ramani hiyo hata kama wewe binafsi una machaguo yako ya tofauti, na kitu cha kushangaza ni kwamba huwa ni vigumu sana kukuta mahitaji ya mtu mmoja yakafanana na mwingine kwa kila kitu, mara nyingi lazima utakuta kuna vitu huvihitaji vipo na ambavyo unahitaji havipo.
Kila mtu huwa na vipaumbele tofauti na mwingine, na hili ni kutoka kwenye uzoefu kwa maana ya kwamba karibu kila kazi tunayokutana nayo huwa ni vigumu kukuta inafanana na kazi ya mtu mwingine kwa vipaumbele vya kimahitaji, achilia mbali utofauti wa ukubwa wa viwanja, utamaduni n.k.,. Unastahili kufanya kitu cha peke yako kinachoendana na vipaumbele vyako.
-Hutaifurahia kazi yako: Kitu ambacho hujaweka akili yako kwenye kuamua kiweje kadiri ya vipaumbele vyako nay ale unayoyapenda huwa ni vigumu kufurahia, hata kama ikitokea ukapenda aina fulani ya jengo au nyumba kutokana na muundo wake, bado kwa ndani kuna vitu hutavifurahia namna jinsi vilivyopangika hivyo unachotakiwa ni kuchukua picha ya lile jengo ulilolipenda na kisha kumuonyesha mtaalamu kumwambia kwamba nataka liwe na muonekano huu kisha alipangilie upya kwa ndani na kuchora upya lakini mwisho wa siku libaki na mwonekano ule unaoupenda wewe.
-Unaweza kujuta sana baadaye: Utakapookoteza ramani, kisha ikajengwa kama ilivyo au hata kama itabdilishwa lakini kienyeji bila kutumia utaalamu sahihi na kushindwa kufikia vile unavyotaka wewe, mara nyingi changamoto zake unakuja kukutana nazo baada ya kuanza kulitumia jengo hilo na hapo ndipo unapokutana na uhalisia ambao hukujihangaisha kuitazama kwa umakini lakini sasa unalazimika kukabiliana nao wakati tayari jengo limekamilika na hapo ndipo utakapojikuta unajuta kwa nini hukuweka umakini mwanzoni au kutafuta mtaalamu wa kukuhakikishia kwamba mambo yanafanyika kwa usahihi, ambapo inaweza kukulazimu sasa wakati huu kutafuta upya mtaalamu kuja kurekebisha changamoto hizo kwa gharama kubwa sana zitakazohusisha kuchora tena, kubomoa na kujenga ili kupata hasa unachotaka.
-Ukikutana na changamoto katikati utashindwa kuitatua: Unapokutana na changamoto wakati wa kujenga, kitu unachofanya na kumwita yule mtalaamu aliyechora kuja kuitatua kwa sababu yeye ndiye mwenye uelewa wa kile alichofanya na ndiye mwenye nakala tete original ya mradi husika kwa ajili ya kufanya mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza, lakini inapotokea sasa umeokoteza ramani pale inapotokea changamoto yoyote ya kiufundi unakuwa huna msaada wa moja kwa moja na wakati mwingine itakulazimu kufanya tena kienyeji kwa ugumu au kuharibu zaidi.
-Unaweza kushtakiwa: Itakapotokea yule aliyefanya kazi husika akagundua kwamba kazi yake inatumika sehemu nyingine bila yeye kujulishwa wala kufahamu chochote anaweza kuchukua hatua za kisheria zitakazokuingiza kwenye gharama pengine kubwa kuliko ambayo ungelipia raani husika.
-Unafanya kosa kisheria na kimaadili: Ni kosa kisheria kutumia kazi ya mtu bila idhini yake na pia kosa kimaadili kutumia kazi ya mtu kwa siri bila mwenyewe kujua kwani unakuwa umemwibia kazi hiyo.
-Kila ramani ina lengo tofauti: Karibu kila ramani inayofanywa na wataalamu huwa ina malengo yake tofauti kutokana na sababu mbalimbli, kwa mfano unaweza kuokoteza ramani ukaijenga kumbe ramani yenyewe ilifanyika katika kiwanja ambacho ni kidogo sana hivyo ikalazimika kuipunguza sana na hata kupunguza baadhi ya vitu muhimu ndani ili iendane na kiwanja husika lakini wewe huna changamoto ya aina hiyo na pengine unahitaji vyumba vyenye nafasi kubwa.
Au pia inawezekana nyumba hiyo ilifanyw akwa ajili ya mtu mwenye familia kubwa na anaishi na wazazi wake pamoja na ndugu wengine lakini wewe una familia ndogo na unaishi na mwenza wako pamoja na watoto wawili peke yake na hivyo huwezi kuwa unaendana na mahitaji yao. Mwisho ni utamaduni wa tofauti, inawezekana wewe ni mtu unayependa kusoma nap engine ungehitahi maktaba ndani ya nyumba wakati huyo mwingine anapenda sinema na anahitaji chumba cha sinema au wewe ni mtu wa maombi sana nap engine ungehitaji chumba maalumu kwa ajili ya sala wakati ramani uliyoiokoteza ni ya mtu anayependa kunywa wine na bia mida ya jioni hivyo alikuwa akihitaji baa ndani ya nyumba.
NB: Umuhimu wa kumtafuta mtaalamu kukufanyia ramani yako mwenyewe inayozingatia vipaumbele vyako ni mkubwa sana hasa ukizingatia kiasi cha fedha unayokwenda kuwekeza kwenye mradi huo ambao mwisho wa siku pia utadumu kwa miaka mingi mbeleni, kwani ramani ya ujenzi inaongeza thamani kubwa sana kwenye nyumba yako na kutoipa kipaumbele sio rahisi kubaki salama.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments