Familia ya kifalme ya Zulu nchini Afrika Kusini imetangaza kifo cha Malkia wake aliyekuwa anaongoza eneo hilo Shiyiwe Mantfombi Dlamini Zulu, mwezi mmoja tu baada ya kutawazwa kuchukua majukumu ya kifalme.
Malkia Mantfombi, 65, alikuwa kiongozi wa mpito wa kabila la Zulu ambalo ndilo kubwa zaidi nchini Afrika Kusini baada ya kifo cha mume wake, Mfalme Goodwill Zwelithini.
Waziri mkuu wa malkia huyo amesema kifo chake kimeshutua familia ambayo ipo kwenye masikitiko makubwa kwa kumpoteza.
Mrithi kama mtawala wa eneo la Wazulu lenye watu milioni 11 bado hajatajwa.
"Ni huzuni na masikitiko makubwa kwamba Familia ya Kifalme inatangaza kifo ambacho hakikutarajiwa cha Malkia Shiyiwe Mantfombi Dlamini Zulu, wa Wazulu," Mwanamfalme Mangosuthu Buthelezi, waziri wake mkuu amesema kwenye taarifa.
Aliongeza kuwa anataka kuhakikishia watu kwamba hakutakuwa na "ombwe la uongozi kwa eneo la Wazulu".
Malkia Mantfombi alilazwa hospitalini wiki moja iliyopita baada ya kuuguwa ugonjwa ambao haukujulikana, kulingana na vyombo vya habari vya Afrika Kusini.
Alikuwa ameteuliwa kuchukua nafasi hiyo Machi 24, baada ya mume wake, 72, Mfalme Zwethilini, kufariki dunia akiwa hospitalini kwa ugonjwa wa kisukari na matatizo mengine.
Mfalme huyo alikuwa ametawala eneo la Wazulu kwa karibu miaka 50 – na kumfanya kuwa mfalme aliyetawala kwa kipindi kirefu zaidi Afrika.
Malkia MaDlamini Zulu alikuwa ameshikilia nafasi ya juu zaidi ya uongozi miongoni mwa wake wa mfalme kwasababu anatoka familia ya kifalme.
Alikuwa dada ya Mfalme wa Eswatini, Mswati III – nchi pekee Afrika ambayo yote inaendeshwa kwa mfumo wa kifalme.
Malkia MaDlamini Zulu na marehemu muwe wake walijaaliwa watoto wanane – ikiwa ni pamoja na vijana 5 wa kiume.
Kijana wao mkubwa, 47, Mwanamfalme Misuzulu, ndiyo mwenye uwezekano mkubwa wa kuchukua uongozi kama mfalme, taarifa zinasema
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments