Mwambusi Atoweka kimyakimya Yanga | ZamotoHabari.




KWA kauli ya kiungwana aliyoitoa ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa sasa ni wazi kuwa aliyekuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi atakuwa rasmi ameachana na klabu hiyo tangu zilipoibuka taarifa zake za kwenda kwao Mbeya kwa ajili ya kuhani msiba wa nduguye.

 

Tangu Mwambusi akabidhiwe mikoba ya aliyekuwa kocha wao, Cedrick Kaze amedumu na kikosi hicho kwa takribani miezi miwili, ambapo ameisaidia timu kuvuna pointi 7, kwenye michezo mitatu aliyohudumu kama mkuu wa benchi la ufundi.

 

Kwani kabla Yanga haijaruhusu kichapo cha pili kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, Jumapili iliyopita timu ikiwa chini ya Mtunisia Nasreddine Al Nabi, kwenye mchezo uliyochezwa Jumapili iliyopita, Mwambusi aliiongoza kupata sare dhidi ya KMC na baadaye akavuna pointi tatu dhidi ya Mtibwa Sugar kisha dhidi ya Gwambina FC.

 

Championi Ijumaa limezungumza na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Haji Mfikirwa ambaye ameweka wazi kuwa, wao kama klabu tayari wameshafanikisha nia yao ya kupata safu mpya ya benchi la ufundi, jambo ambalo liliwafanya wamuombe Mwambusi kukaimu nafasi hiyo.

 

“Kikubwa unachotakiwa kufahamu ni kwamba, timu tayari ipo chini ya kocha wetu mpya, ambaye tayari ameshaanza kazi, hatukuwa na sababu ya kumzuia kutumia muda wa mapumziko yake kwenda msibani, jambo la msingi ni kwamba alifiwa na mtu muhimu kwake, anatumia muda huo kupumzika hadi pale atakapokuja tutaona cha kufanya,” alisema Mfikirwa.

 

Gazeti la Championi Ijumaa lilimtafuta Mwambusi ili azungumzie safari yake hiyo ambapo alisema: “Kama ulivyotaarifiwa ni kweli nipo msibani na ninaomba sasa uniache nitumie muda huu kupumzika.”

Stori: Musa Mateja, Dar es Salaam



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini