Saa 7 kamili mchana, siku ya jumapili ya tarehe 1.11.1987, Watanzania, kila pembe ya nchi, walipigwa butwaa na kushikwa na bumbuwazi kubwa baada ya Radio Tanzania Dar Es Salaam kutangaza, katika taarifa ya habari, kwamba mwanamke aitwae SARAH MARTIN SIMBAULANGA (35) mfanyakazi wa NBC alikuwa amekwapua mamilioni ya fedha na alitoroka nchini akiwa na watoto wake watatu na laaziz wake, Mfanyabiashara TOROHA MOHAMED TOROHA(40).
Tukio hilo la kipekee na la aina yake liliwaacha midomo wazi wananchi hasa kwavile enzi hizo halikuwa jambo la kawaida kwa mwanamke kuwa "mpigaji" wa kiwango cha kutisha cha fedha nyingi kiasi kile!.
Tukio hilo liliongelewa mno sehemu mbalimbali hasa maofisini, majumbani, mashuleni, masokoni, mahotelini, vilabuni nk huku wengi wakimlaani vikali mwanamke huyo na kusikitika nchi kuibiwa fedha nyingi kiasi hicho. Kwa wengi, ilikuwa ni simanzi kubwa sana na haikushangaza basi pale Mkutano Mkuu wa Baraza la Kuu la vijana uliokuwa ukifanyika Singida kutoa wito kuwa uongozi wote wa juu wa NBC "Ufyekelewe mbali"!.
Ofisi ya DCI, mara moja, ilituma taarifa (Interpol) nchi mbalimbali ili zisaidie kuwakamata "mabandido" hao.
Hatimaye, majira ya saa 9 alasiri, siku ya Ijumaa, tarehe 13.11.1987, Bw. TOROHA akabambwa kwenye ofisi ya magari ya Toyota jijini Nairobi, Kenya akiwa kwenye mishemishe ya ununuzi wa magari.
"Mandata" walipombana aeleze kuhusu aliko Bi. SARAH, Bw. TOROHA hakuwa na namna zaidi ya kuwapeleka chumba na. 322 cha hotel maarufu ya Jacaranda. "Mandata" hao, wakiwa na TOROHA, waliingia chumba hicho na kumkamata Bi. SARAH kiulaiiini!.
Jijini Dar Es Salaam, NBC ilimfukuza kazi Bi. SARAH kwa kutoonekana kazini kwa siku 5 mfululizo. Aidha, kamatakamata ilianza ambapo wafuatao walikamatwa na kuhusishwa na wizi huo: Bw. ROMANIUS PETER NDANZI(43), Mdhibiti wa Fedha za Kigeni, NBC "Foreign Branch", Bw. ERNEST JOHN MWENEWANDA(40), Meneja mauzo KLM, HAROON DAUD(35), Mfanyabiashara. Washtakiwa hawa, tarehe 19.11.1987, walifikishwa Kisutu kwa "Pilato" Mh. JUMA MUSTAPHA JIBREA. Waliomba dhamana wakanyimwa. Wakakata rufaa Mahakama Kuu. Tarehe 5.1.1988, Jaji LUHEKELO KYANDO, aliwanyima dhamana na kueleza, kwa uchungu na uzalendo, kwamba:
*"Kiini cha kesi hii ni moja ya matukio ambayo yameshtua sana umma kuona kwamba mamilioni ya fedha yanaibwa. Ni maoni yangu kuwa itakuwa kinyume na hisia za jamii ikiwa mahakama itachukua msimamo tofauti na usiokuwa na mwelekeo wa hisia sahihi kuhusu vitendo hivi"*.
Msimamo huu uliakisi kilichoelezwa na aliyekuwa Waziri wa sheria, Mama JULLIE MANNING, tarehe 17.1.1988, kwamba: *"Ingawa Mahakama hazipendelei upande wowote, hiyo haina maana kwamba zisijali nini kinatokea nchini"*.
Serikali ilituma Kenya Hati ya kuomba SARAH na TOROHA warudishwe nchini(Extradition) kwani nchi hizi zina makubaliano hayo ya aina hiyo. Hati hiyo iliwasilishwa na SP PETER MWANGI mahakamani saa 2.30 asubuhi ijumaa, tarehe 15.1.1988 mbele ya Hakimu Mwandamizi, Mh JOSEPH MANGO na kisha maombi hayo yakaanza kusikilizwa.
Tarehe 29.11.1987, mahakama hiyo ikatoa uamuzi kuwa, kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, SARAH arudishwe Tanzania kujibu mashtaka lakini ikamuachia huru TOROHA. Baada tu ya kuachiwa, mbio alizotimua TOROHA, hata USAIN BOLT angesubiri!.
Siku ya jumanne, saa 6 mchana, tarehe 2.2.1988, SARAH alikabidhiwa kwa maafisa wa Tanzania mpakani Namanga na kukimbizwa "wanguwangu" na magari 5 ya polisi hadi Dar Es Salaam.
SARAH alifikishwa mahakama ya Kisutu saa tatu asubuhi, siku ya Jumatano, tarehe 10.2.1988 chini ya ulinzi mkali. Mahakama hiyo ilikuwa imefurika mno huku barabara ya Bibi Titi ikifungwa kwa muda kwani wananchi wengi walitoroka makazini kwenda kumuona SARAH anafananaje na kusikia aliwezaje kuiba kitita chote hicho!.
Mbele ya Hakimu Mwandamizi Mh. JOSEPH MASANCHE, Bi. SARAH alisomewa mashtaka 5 na SSP EDWIN ABRAHAM MAN. Bi. SARAH alikuwa akitetewa na Dr. MASUMBUKO ROMAN LAMWAI, mmoja wa mawakili bora kabisa kuwahi kutokea nchini.
Bi. SARAH aliushangaza umati uliofurika, pale bila kupepesa macho, kutingisha pua wala kutikisa maskio, alipokiri mashtaka yote 5! Hakimu MASANCHE nae pia alipigwa butwaa na ikabidi amuulize kama ameelewa vizuri mashtaka ambapo "alikomaa" na kusema anaelewa na anakiri ni kweli alienda makosa hayo!.
Mh MASANCHE, baada ya kusikiliza pande zote 2 kuhusu adhabu, akasoma hukumu iliyochukua robo saa tu ambapo alimuhukumu SARAH kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa na makosa yote kwenda pamoja hivyo angetumikia miaka 7 tu na pia akamuamuru arudishe fedha hizo mara moja. Mh MASANCHE alin'gaka- *"Hakuna kitu kibaya kama wizi wa fedha za kigeni ambazo Taifa linazihitaji sana"*.
Upande wa mashtaka hakuridhika na adhabu hiyo "kiduchu" hivyo ukakata rufaa Mahakama Kuu kuomba adhabu hiyo iwe kwa kufuatana na sio kwa pamoja. Aliyekuwa Jaji Kiongozi, Mh. NASSOR MZAVAS ndiye aliyesikiliza rufaa hiyo huku jamhuri ikiwakilishwa na Bw. KULWA SATO MASSABA na Dr. LAMWAI akimuwakilisha SARAH.
Saa 4 asubuhi, Ijumaa ya tarehe 19.2.1988, Mh MZAVAS alitoa hukumu. Baada ya kuisoma hukumu hiyo kwa dakika 45, huku umati ukisubiri kwa hamu, Mh. MZAVAS "aliinama na kujifanya kama anajikuna" kisha "akampiga SARAH mvua 28"! SARAH hakuamini macho yake na kubaki amebun'gaa! Mh. MZAVAS akamalizia- *"Hii ni hasara ya kiuchumi ambayo inaiathiri nchi. Fedha hizo kidogo za kigeni nchi ilizofaulu kujiwekea akiba kwa kujikidhi sana, ndio inalolifanya kosa la kuiba fedha za kigeni kutisha. Wizi huu ulipotangazwa na RTD, Mahakama pia ilisononeka na kufadhaika sana kwa kuibwa kwa fedha hizo za kigeni kwani Mahakama nayo ni sehemu ya jamii"*.
"Upigaji" huu wa ulikuwa umepangwa na wapenzi hao wawili, SARAH na TOROHA. TOROHA alikuwa ni kijana mtanashati aliyezaliwa Mbegani, Bwagamoyo mwaka 1948. Baba yake aliwahi kufanya kazi Ikulu na kisha akawa Afisa wa ubalozi Japan na Uholanzi miaka ya mwanzoni ya Uhuru na alikuwa na uwezo wa kifedha. Mwaka 1967, baada ya kuzinguliwa na siasa ya Ujamaa ambapo nyumba yake ilitaifishwa, aliacha kazi na kutimkia Ujerumani na kufanya biashara ya mkahawa na duka la vinyago.
Mwaka 1979, Bw. TOROHA, akiwa kijana wa miaka 31, alimuoa Mkenya, Bi. ELIZABETH WANJIRU na wakaishi Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia na Kenya.
TOROHA alikuwa akija nchini mara mojamoja hivyo akaanza urafiki na Bi. SARAH aliyekuwa binti mdogo mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Zanaki jijini. SARAH, baadaye, aliajiriwa NBC na kupanda vyeo hadi kuwa Msimamizi, Idara ya Fedha za Kigeni.
TOROHA aliingia nchini tarehe 11.10.1987 na kufanya "mchongo wa upigaji" na "Mpango wa kando" wake, Bi. SARAH. Ili kufanikisha dili la upigaji na kusepa nje ya nchi bila kushtukiwa, Bi. SARAH alishirikiana na maafisa wasio waaminifu wa "Immigration" na kubadili majina yake na ya wanawe na kupata "passports" mpya tarehe 28.10.1987. "Passport" ya SARAH yenye Na. 220130 ikawa na jina KHADIJA ALI MKIMBAU. "Passports" za wanawe zikawa na majina mapya 1.HAPPINESS SIMBAULANGA-(JAMILA ISMAEL HASSAN), 2. SIMBA SIMBAULANGA- (HALFAN ISMAIL HASSAN), 3. BLANDINA SIMBAULANGA-(JENIPHER ISMAEL HASSAN).
Kisha, SARAH "akapiga" hundi za kusafiria 1,100 zenye thamani ya $ 390.000 na hundi 200 zenye thamani ya £ 20.000. Fedha hizo 'alizipiga' mara 3 kati ya tarehe 19.10.1987 na 29.10.1987. Kwa wakati huo, hizo zilikuwa ni fedha nyingi sana. Baada ya mchongo kukamilika, SARAH na TOROHA walichukua vyumba 2 katika hotel maarufu sana ya Skyway iliyokuwa makutano ya Ohio na Samora. Chumba kimoja kilikuwa chao na kingine cha watoto wa SARAH ambako walilala kwa usiku mmoja wa Ijumaa, tarehe 30.10.1987. Usiku wa Ijumaa hiyo, SARAH na TOROHA walienda ukumbi wa White House "kushangilia ushindi" ambako bendi ya Marquis du Zaire chini ya Babu Seya iliwapagawisha vilivyo!.
Tarehe 31.10.1987, TOROHA, kin'gast chake SARAH na watoto wake 3 walikwea pipa la ATC kwenda Kenya. Walipotua tu Jomo Kenyata International Airport, wakatumia hundi zenye thamani ya $ 2700 kununua tiketi 5 za KLM na wakaenda Amsterdam na kisha London. Wakiwa London UK, waliofanya "transactions" nyingi "Baclays bank" na tarehe 2.11.1988 wakanunua tiketi 5 za KLM ili waondoke kuelekea Kenya tarehe 5.11.1987. Tarehe 3 na 4 ilikuwa ni "kujirusha" tu nchi ya Malkia ie *Kazi na Bata*!.
Tarehe 5.11.1987 walikwea KLM na kufika Kenya tarehe 6.11.1987. Nchini Kenya walifanya matanuzi na manunuzi ambapo TOROHA alitumia $ 260,000 kununua magari (mini-bus 4 na pick up 1) na yote akayasajiri kwa jina la SARAH. TOROHA, alipokuwa akitaka kununua magari mengine ndipo aliponyakwa na mamwela katika ofisi za Toyota tarehe 13.11.1987! .
Huu ndio mkasa wa Bi. *SARAH MARTIN SIMBAULANGA* @khadija ALLY MKIMBAU uliokuwa wa aina yake na wa kipekee!
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments