Na Amiri Kilagalila,Njombe
Ni katika kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya kikiongozwa na Mwenyekiti wake Bi Ruth Msafiri ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo agenda kuu ikiwa moja ya kuipandisha Halmashauri ya Mji Njombe kuwa Manispaa ambapo wajumbe wa kikao hicho wamepongeza mapendekezo hayo na kuridhia uamuzi huo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kufikia lengo hilo.
Akiwasilisha rasimu ya mapendekezo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi Illuminatha Mwenda amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Halmashauri mwaka 2007,Halmashauri ya Mji Njombe imekuwa ikijitahidi katika kuboresha utoaji huduma kwa kuzingatia misingi na miongozo ya kuundwa kwake ikiwa ni pamoja na uzingatiaji sheria, utawala bora na usimamizi wa makusanyo na matumizi ya fedha katika kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi jambo lililopeleka menejimenti kuona kuwa kwa sasa Halmashauri inaweza kutoka katika hadhi ya Mji Kuwa Manispaa.
Bi Mwenda aliendelea kufafanua kuwa Halmashauri imeendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato ambapo imekuwa kati ya Halmashauri za miji zilizo na wastani wa kukusanya Shilingi Bilioni 4 kwa mwaka na imekuwa juu ya manispaa 10 na Halmashauri za Miji 24 ambazo hukusanya wastani wa Shilingi Bilioni moja hadi tatu kwa mwaka na hivyo kuweza kukidhi kigezo cha Manispaa.
Mwenda aliendelea kusema kuwa yapo maeneo yanayohitaji kuendelea kuboreshwa ambapo ni kuongezwa kwa mtandao wa barabara za lami,kuthibiti ujenzi holela,kuhimiza ujenzi wa majengo ya ghorofa uthibiti wa upakiaji na ushushaji holela wa abiria sambamba na utoaji wa huduma za maji safi na maji taka.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amesema kuwa kwa sasa Halmashauri ya Mji Njombe imeweza kupiga hatua kubwa na kuweza kusimamia malengo yake ipasavyo jambo linalopelekea kwenda kwenye hatua nyingine.
“Dosari ndogondogo zinaweza kuwepo ila zisitufanye tushindwe kusonga mbele kutoka kuwa Mji kwenda Manispaa. Tukiwa Manispaa tunapata faida nyingi kuliko hivi tulivyo. Mwonekano,fikra na utendaji wetu utakwenda kubadilika. Tuihamasishe, kuielimisha na kuishajihisha jamii kuipokea Manispaa” Alisema Msafiri
Wakitoa mapendekezo yao katika kikao hicho baadhi ya wajumbe wamepongeza jitihada zinazofanywa na viongozi hao katika kuleta maendeleo kwenye Mkoa wa Njombe na wameitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa jambo hilo linafanyika kwa haraka ili jamii iweze kunufaika na mabadiliko hayo.
Wakichangia kwenye baadhi ya changamoto zilizobainishwa ambazo zinatakiwa kufanyia maboresho Mwakilishi kutoka TARURA amesema kuwa Halmashauri kwa kushirikiana nao wameweza kuandika andiko la kuomba barabara kupitia mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo wanataraji kupata mtandao wa barabara za lami ndani ya Halmashauri ambapo zitasaidia kutatua changamoto hiyo ya ukosefu wa barabara zenye viwango vya lami kwenye eneo la Mji.
Katika kuboresha huduma za utoaji maji safi Meneja NJUWASA Na RUWASA wamesema kuwa kwa sasa ipo miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na mingine imekamilika na kuanza kutoa maji katika maeneo mbalimbali ambapo kwa upande wao NJUWASA matarajio yao ni kuanza kwa mradi wa maji wa Hagafilo unaotaraji kuanza mara baada ya kukamilika kwa tathmini zote mradi ambao utasaidia wakazi wa njombe kupata maji ya kutoka kwa miaka 20 ijayo
Kuhusu majenzi holela na ujenzi wa majengo ya Ghorofa kwenye eneo la kibiashara CBD wadau hao wamesema kuwa ni vyema matumizi ya mpango kabambe wa Halmashauri (Master Plan) ambao upo tayari ukawekwa wazi na kutangazwa kwa Wananchi wote ili kila mtu apate elimu ya nini kinatakiwa kujengwa katika eneo gani badala ya kila mtu kujenga holela jambo ambalo litapelekea kushindwa kuwa Manispaa mpya ya mfano.
Aidha wamesisitiza kuwa katika maeneo ya Mjini kwenye Kata tatu ni vyema Wananchi wenye uwezo wahamasishwe kujenga nyumba za ghorofa ili kuweza kuleta madhari nzuri na kuondoa ujenzi uliozoeleka.
Kuhusu uwepo wa vituo vya upakiaji na ushushaji abiria holela kikao hicho kimeridhia kurejelea tena makubaliano yaliyofikiwa katika vipindi vya nyuma na kurudisha utaratibu wa awali uliokuwa ukitumika na kuhakisha kuwa stendi ya mabasi inatumika kama ilivyokuwa mwanzo.
Wadau hao wameafiki na kupongeza hatua hizo ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo alitoa maazimio ya kuundwa kwa timu ya uhamasisha ambayo itaenda kuhamasisha jamii na kutoa elimu kwa jamii kuona umuhimu wa kuwa Manispaa sambamba na kuwa na mpango kazi ambapo pamoja na hayo imeweza kuundwa timu kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo hayo katika ngazi ya Mkoa.
Kwa mujibu wa vigezo na tathmini Halmashauri ya Mji Njombe ipo katika hatua za awali kuipandisha Halmashauri kutoka Mji kwenda Manispaa.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments