MKOA WA PWANI YASHUSHA KIKOSI CHA WACHEZAJI 100 KUSHIRIKI MICHUANO YA TAIFA UMITASHUMTA MTWARA | ZamotoHabari

JUMLA ya wachezaji wapatao 100 wamechaguliwa kwa ajili ya kuweza kuunda kikosi cha timu ya Mkoa wa Pwani ambacho kitashiriki katika kinyanga’nyoro cha michezo mbali mbali kwenye kivumbi cha Mashindano ya umoja wa michezo na taalumu kwa shule ya za msingi (UMITASHUMTA) ngazi ya Taifa ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake mwanzoni mwa mwezi huu Mkoani Mtwara.

Hayo yamebainishwa na Afisa Michezo wa Mkoa wa Pwani Grace Buleta wakati wa kufunga rasmi michuano ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa na kubainisha kuwa kabla ya kuchagua kikosi hicho cha wachezaji 100 kuliweza kufanyika mashindano katika michezo mbali mbali ambayo yaliweza kuwajumuisha wanamichezo kutoka halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani na ndipo jopo la kamati ya michezo kwa kushirikiana na maafisa michezo waliweza kuwachagua wachezaji kwa kuzingatia vigezo.

Buleta aliongeza kuwa hapo awali wachezaji ambao walishiriki katika mashindano ya ngazi ya Mkoa kwa ajili ya kupata kikosi hicho walikuwa zaidi ya 650 lakini kwa sasa baada ya michuano hiyo kumalizika waliweza kuwachagua baadhi ya wachezaji ambao wana vipaji na uwezo kwa lengo la kuweza kuunda kikosi cha Mkoa kilichokuwa bora.

“Tunashukuru hii hatua ya mwanzo tumeweza kuikamilisha ya kupata wachezaji 100 ambao wataunda timu ya Mkoa wa Pwani na kwamba sio kwamba wengine hawana uwezo lakini tumehakikisha kwamba tunawachagua wale wachazaji ambao wameweza kuonyesha uwezo wao katika kipindi chote za mashindano hayo na nia yetu kubwa ni kufanya vizuri katika mashindano ya Taifa,”alisema Buleta.

Aidha Buleta alifafanua kuwa kwa sasa mipango ambayo wameiweka ni kuiweka timu ya Mkoa kambini kwanza kwa muda nne hadi kwa ajili ya kuweza kuwapa fursa walimu na makocha waweze kutoa maelekezo mbali mbali ambayo yatawasaidia wachezaji kujifunza mambo mbali mbali ikiwemo sheria na taratibu ambazo zitakwenda kutumika katika mashindano ya Taifa.

“Zoezi la kuchagua kikosi cha timu ya Mkoa wa Pwani kwa upande wetu tumelifanya kwa kuzingatia usawa katika kila pande na kwamba katika michuano hii tumeweza kuwachagua wachezaji katika michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa mikono, netiboli, Riadha, mpira wa wavu, pamoja na fani mbali mbali za ndani ikiwemo ngoma na kwaya.”alifafanua Buleta.

Katika hatua nyingine Buleta aliongeza kwamba katika michuano ya msimu wa mwaka huu wa 2021 wamejipanga vizuri hivyo wanatarajia kuipeperusha vema bendera ya Mkoa wa Pwani na kurudi na ubingwa na kuwaomba wadau, mashirika na umma na taasisi binafsi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa sapoti ya hali na mali kwa kikosi hicho kilichoundwa cha Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha injinia Martine Ntemo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mashindano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amewataka wanamichezo hao kuhakikisha kwamba wanajitadi kwa uwezo wao wote kufanya vizuri katika mashindano hayo ya Taifa kwa lengo la kuweza kuibuka na ubingwa na kurudi na vikombe ili kuutangaza vema Mkoa wa Pwani katika Nyanja ya michezo.

Pia Ntemo aliwasisitizia kwamba wanamichezo ho hao kuhakikisha wanachukua tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa mbali mbali na kuziagiza halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya viwanja vya michezo kwa wanafunzi hao sambamba na kuwanunulia sare za michezo na kuwataka pia wanafunzi hao kuwa na nidhani katika kipindi chote na michuano hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la elimu Kibaha Robert Shilingi akitoa salamu zake alisema kuwa wachezaji wote ambao wamechagulia kunda kikosi cha timu ya Mkoa kupambana vilivyo na kutumia fursa hiyo katika kuonyesha vipaji uwezo walionao katika michuano hiyo ya ngazi ya taifa ili kurudi na ubingwa ambao utaweza kuwa na tija zaidi katika sekta ya michezo ndani ya Mkoa wa Pwani.


Baaadhi ya wanafunzi kutoka katika shule mbali mbali kutoka halmashauri mbali mbali wakiwa wanashangia baada ya kumalizika kwa mashindano hayo ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa wa Pwani ambayo yamefanyika katika viwanja vya shirika la elimu Kibaha, na hatimaye kuchaguliwa kwa wachezaji wapatao 100 ambao wataunda kikosi cha timu ya Mkoa wa Pwani.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Injinia Martine Ntemo akizungumza na wanamichezo, walimu, maafisa michezo na utamaduni wakati wa halfa ya kufunga michuano hiyo ya shule za msingi UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa wa Pwani ambapo pia ilihudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali na wakuu wa idara.

Afisa michezo wa Mkoa wa Pwani Grace Buleta kushoto akiwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakati wa hafla hiyo ya kufunga mashindano hayo ya wanafunzi wa shule za msingi UMITASHUMTA ambayo yamefungwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Injinia Martine Ntemo.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini