Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Wilaya ya Kisarawe kupata bahati ya kujengewa Uwanja wa kisasa wa mchezo wa mpira wa Kikapu utakaojengwa katika Shule ya Sekondari ya Minaki iliyopo Wilayani humo kupitia mradi wa Giants of Africa chini ya uongozi wa Masai Ujiri.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Wilayani humo, Dkt. Kikwete ameipongeza Wilaya ya Kisarawe kwa kukaribisha Ujenzi wa Uwanja huo utakaonufaisha Shule ya Sekondari Minaki na Shule zote za jirani.
Dkt. Kikwete amesema Ujenzi wa Uwanja huo utashawishi Wanafunzi na Vijana Wilayani humo kuupenda mchezo huo wa mpira wa Kikapu ambapo baadae utasaidia kukuza vipaji tofauti kwa manufaa ya Taifa la Tanzania kupitia mchezo wa Basketball.
“Nimefurahi kufika Shule ya Sekondari Minaki, tulikuwa tunakuja hapa kucheza Basketball kipindi kile nasoma Kibaha Sekondari, shukrani sana kwa Giants of Africa (GOA) wamefanya jambo kubwa sana kwa manufaa ya vipaji vya vijana wa Wilaya ya Kisarawe na Tanzania kwa ujumla”.
“Kufanikisha Ujenzi wa Uwanja huu hapa Minaki, viongozi wa mpira wa kikapu jitahidini wanapokuja Wachezaji wakubwa wa mpira huu (Basketball) mnawatangaza ili nchi ijue kuwa kuna Mchezaji fulani kaja, hii itasaidia vijana wetu kuupenda mchezo huu kusaidia kupata timu nzuri ya Taifa”, amesema Dkt. Kikwete.
Aidha, Dkt. Kikwete amewaasa Viongozi Wilayani Kisarawe na Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini kuwaandaa Wakufunzi wa mchezo huo kufanikisha kupata vipaji vya mchezo huo kwa Wilaya za Kasarawe na mkoa wa Pwani sambamba na Taifa kwa ujumla.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amewashukuru wadau wa mchezo wa mpira wa kikapu kufanikisha Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa, amesema Wilaya ya Kisarawe wanajivunia kupata Uwanja huo utakaosaidia Wanafunzi na Vijana wilayani humo katika mchezo huo.
“Naamini kupitia Uwanja huo, vipaji vya vijana wetu vitaonekana na baadae itatuweka katika ramani ya mchezo wa mpira wa Kikapu kimataifa, tunashukuru pia kupata baraka za Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Kikwete katika kukamilisha mrasi huu hapa Kisarawe”, ameeleza DC Jokate.
Mwakilishi wa Giants of Africa (GOT) katika maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Abel Nson amewashukuru watu wa Kisarawe kushirikiana nao katika kufanikisha ujenzi wa Mradi huo utakaokamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, amewashukuru Dkt. Kikwete na DC Jokate kwa ushawishi wao mkubwa kuwaleta hapo ili kukuza vipaji vya Wachezaji wa Basketball Kisarawe.
Pia, Rais Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa amesema Ujenzi wa mradi huo wa Uwanja wa kisasa ni fursa kwa vijana wa Tanzania kukua katika mpira wa kikapu na kufika mbali kupitia mchezo huo kama walifanya kina Hasheem Thabit.
Magesa amesema kupitia mchezo huo wa kikapu Shirikisho hilo linatoa ufadhili wa masomo (Scholarship) kwa vijana wote wanaofanya vizuri zaidi kwenye Masomo yao na kucheza vizuri mchezo huo wa Basketball.
Mradi huo wa ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa Mpira wa Kikapu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu na unatekelezwa na Giants of Africa chini ya uongozi wake Rais wa Timu ya Toronto Raptors, na Mchezaji maarufu wa mchezo huo, Masai Ujiri.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments