SERIKALI KUENDELEA KUFANYA TAFITI ZA MALISHO YA MIFUGO NCHINI | ZamotoHabari.


Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto) akielezea namna Wizara inavyojipanga kushirikiana na shirika la kimataifa la Heifer kwenye shughuli za Utafiti muda mfupi baada ya kutembelea banda la shirika hilo leo (02.06.2021) kwenye maonesho ya wiki ya Maziwa yanayofanyika kwenye viwanja vya Tangamano jijini Tanga, Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Shirika hilo anayesimamia mradi wa usindikaji maziwa Mark tsoxo (katikati) na kiongozi wa miradi kutoka Shirika la kimataifa la CIAT ambalo linaratibu mradi wa utafiti wa malisho yanayozingatia utunzanji wa mazingira, An Notenbaert.
Mkuu wa kituo cha Utafiti wa Mifugo (TALIRI) kampasi ya Tanga, Dkt. Zabron Nziku (kulia) akiwaonesha wafugaji na wazalishaji wa malisho kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro picha yenye aina tofauti za nyasi aina ya “brachiaria” zinazopatikana kwenye mashamba ya Taasisi hiyo wakati timu hiyo ilipotembelea mashamba hayo.
Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Angelo Mwilawa (aliyechuchumaa) akitoa maelezo kuhusu malisho ya nyasi aina ya “buffel au “Cenchrus ciliaris” kama yanavyojulikana kitaalam wakati wa ziara ya wafugaji na wazalishaji wa malisho kutoka Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro iliyofanyika kwenye ofisi za Taasisi ya Utafiti wa mifugo (TALIRI) jijini Tanga.


MKURUGENZI wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa amesema kuwa Serikali inakusudia kuendelea kufanya utafiti zaidi wa malisho ya mifugo baada ya kuona matunda ya tafiti ambazo zimeshafanyika.

Dkt. Mwilawa amesema hayo leo (02.06.2021) jijini Tanga kwenye Mashamba ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) alipokuwa akiongoza timu ya wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro ambao walifika kwenye mashamba hayo kwa lengo la kujifunza juu ya aina mbalimbali za mbegu za malisho yanayostawi maeneo yenye mvua na yale yanayostahimili ukame.

“Kiu kubwa ya Serikali ni kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa malisho kwa wafugaji wetu inamalizika kabisa na tunapata faraja kubwa pale tunapowaona wafugaji wetu wananufaika na matunda ya tafiti mbalimbali za malisho ambazo tumekuwa tulizifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali” Amesema Dkt. Mwilawa.

Aidha Dkt. Mwilawa amebainisha kuwa ziara hizo za wafugaji zitaisaidia Serikali kupata maoni yao juu ya mambo ambayo wangependa yafanyiwe kazi ili waendelee kuwa na ufugaji na uzalishaji malisho wenye tija na utakaowanufaisha zaidi.

“Napenda niwashukuru wadau wetu ambao wamekuwa nasi katika kufanikisha tafiti mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wafugaji wetu likiwepo shirika la “CIAT” na sisi kama Serikali tunawaahidi tutaendeleza yale ambayo wametusaidia hata mara baada ya mradi kuisha” aliongeza Dkt. Mwilawa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Suzana Nyagawa ambaye ni mfugaji kutoka mkoa wa Njombe amesema kuwa amefurahishwa na nyingi za malisho ya mifugo alizozikuta shambani hapo ingawa amebainisha kuwa changamoto ya hali ya hewa ya baridi iliyopo kwenye mkoa wake ni moja ya changamoto zinazofanya aina nyingi za malisho zisistawi vizuri.

“Kutokana na changamoto hiyo huwa tunakata malisho tuliyoyapata wakati wa masika kisha tunayakata na kuhifadhi ili yatusaidie wakati wa kiangazi” ameongeza Nyagawa.

Kwa upande wake Gwamaka Mwakiambiki ambaye ni mfugaji kutoka Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, amesema kuwa jambo alilojifunza mara baada ya kufika shambani hapo ni kuzalisha aina nyingi za malisho ya mifugo badala ya kutegemea aina moja tu ya majani aina ya “brachiaria” ambayo ndio yanayostawi vizuri katika mkoa wake.

“Tunalishukuru sana shirika la CIAT kwa sababu tangu lilipokuja tumejifunza namna ya kupanda malisho bora na yanayoipa mifugo yetu afya bora” alihitimisha Mwakiambiki.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikishirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwenye tafiti za malisho ya mifugo ikiwa ni jitihada za kumaliza changamoto ya malisho ya mifugo nchini.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini