Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa kutetea Haki za Binadamu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kama ilivyohainishwa katika katiba na ilani ya chama cha mapindizi (CCM) ya mwaka 2020/2025.
Akizungumza na watumishi wa Mtandao wa Kutetea Mashirika yanayotetea haki za Binadamu (THRDC) Waziri wa Katiba na Sheria Prof Palamagamba Kabudi amesema Serikali haina budi kushirikiana na wadau wenye nia ya kutetea wananchi na hasa wanyonge.
"Tuko tayari kushirikiana na wadau ninyi muhimu kwenye masuala ya kupigania haki za wananchi tunajua kuwa mtakua na vipaumbele vyenu muhimu na serikali pia itakuwa na vipengele vyake ambavyo vinalenga kukuza haki za binadamu nakuleta maendeleo katika nchi yetu,
"Hayo yote ni matakwa ya ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kuwa serikali imeahidi kuheshimu na kuzingatia haki za binadamu kwa mtu mmoja mmoja, makundi na makundi ili kujenga jamii yenye usawa," Amesema Waziri Kabudi.
Amesema Tanzania sio nchi ya kufundishwa kupigiania haki za binadamu kwani ni suala ambalo lilianza tangu zamani sana na kila kitu kimeandikwa kwenye katiba.
Kwa Upande wake Mratibu wa Mtandao wa THRDC Onesmo Olengurumwa amesema serikali inatambua kuwa mfumo bora wa sheria ndio msingi wa kutekeleza matakwa ya katiba, sera na mpango wa nchi.
Amesema asasi za kutetea haki za binadamu zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamiii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.
"Asasi za kiraia zimekuwa zikifanya vizuri sana hapa nchini tunaomba serikali itambue mchango wa asasi hizo na kuongeza ushirikiano ili zziendelee kufanya vizuri kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla," Amesema.
Olengurumwa ameihakikishia serikali kuwa mashirika ya kutetea haki za binadamu yataendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati bila vipingamizi vyovyote.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments