Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WAJASIRIAMALI nchini na Zanzibar wameiomba serikali kuangalia kero wanayoipata kupitia vifungashio ambavyo vimepigwa marufuku kutumika ambavyo baadhi yao wamekuwa wakipata hasara kwa kuviagizia kutoka nchini China hasa kwa upande wa Zanzibar.Akiongea mbele ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe kwa niaba ya wengine mjasiriamali kutoka Zanzibar Dadi Ahmedi Dadi alisema Tanzania Bara kuna viwanda vidogo vidogo vingi na vinatambulika lakini kikwazo kikubwa ni upatikanaji wa vifungashio nchini.
"Kwanza niseme salamu za wajasiriamali katika maonyesho ya biashara ya nane hapa Tanga, kitu cha kwanza kinachotukwamisha wajasiriamali ni vifungashio, jambo hili mimi binafsi katika kiwanda changu cha usindikaji wa matunda na mbogamboga toka nilivyoanza nilikuwa naweka oda kule China, tuna viwanda vingi Tanzania Bara lakini tunakuwa na vikwazo kwa kiwango kikubwa cha kwenda kulipia ili kupata vifungashio" alisema.
"Muheshimiwa Naibu Waziri naomba hili mliangalie kwa macho mawili, tunapata shida Wanzazibar, tunapata shida Watanzania kwa ujumla, kwa ushahidi nilionao, niliagiza mzigo wa vifungashio vya bidhaa tatu nilitakiwa nitoe shilingi milioni kumi, sasa milioni kumi kwa mjasiriamali tukisema tunaanza na vifungashio hii malighafi itanunuliwa kwa kitu gani, hili ni suala gumu sana kwetu" aliongeza Dadi.
"Ili kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda na biashara serikali haina budi kuangalia eneo la viwanda vidogo vidogo na vya kati kupata vifungashio, hiki ndio kikwazo kikubwa sana kwetu sisi" alisisitiza.
Hata hivyo alisema kikwazo kingine ni katika kupatiwa mikopo katika Taasisi za kibenki ambako hata ukiwa na vigezo vya kibiashara bado kuna suala la kukosa hatimiliki ambalo kwa upande wa visiwani ni tatizo kubwa hasa katika maeneo ya biashara.
"Kwa ushahidi nilionao muheshimiwa, hii taasisi ya benki ya CRDB kule Pemba ilivyoanza kazi tuliona ni benki nzuri sana, lakini katika kupata mikopo imekuwa ni kikwazo kikubwa kutokana na mashariti magumu wanayotuwekea, kwenye kiwanda changu meneja wa benki alikuja kututembèlea na akakuta bidhaa tulizonazo alifarijika sana na akaona tunafaa kukopesheka, lakini kikwazo kikubwa hatuna dhamana"alieleza.
"Watanzania au hasa visiwani tumekuwa na tatizo la kutokuwa na hati miliki katika maeneo ambayo ni dhamana zinazohitajoka katika Taasisi za kifedha, hivyo tunaomba serikali kuweka sera inayotekelezeka kuhusu mikopo ili tuweze kukopeshwa, katika mazingira hayo ya kifedha tunahitaji kuzalisha vitu vizuri" aliongeza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu vikwazo vya wajasiriamali Naibu Waziri Exaud Kigahe alisema viwanda vingi nchini ni vya uchakataji mazao ya kilimo jivyo kuna haja ya kuongeza thamani mazao hao na kuongeza kuwa kikwazo cha vifungashio siyo tu viwanda vidogo bali hata kwa viwanda vya kati.
Kigahe alibainisha kwamba vifungashio ni sehemu ya ubora wa bidhaa na kukiri kuwepo kikwazo cha mikopo na kwamba katika maonyesho hayo serikali imechukua jukumu la kualika Taasisi zote za kibenki ili kuwezesha wajasitiamali wadogo kipata mikopo kwenye Taasisi zao ikiwa ni pamoja na kupitia kwenye Mashirika kama SIDO ambao pia wanakopesha kupitia mifuko ya wananchi.
"Ndugu zangu viwanda vingi vya Tanzania ni vile vinavyohusiana na uchakataki wa mazao ya kilimo, na ndivyo ambavyo tunaviona hapa, nitoe pongezi kwa wenzetu ambao wana mashine zinazotumika kuongezea thamani ya mazao, kimsingi maonyesho haya yamekuwa kichocheo kikubwa kwa mkoa wa Tanga" alisema.
Sambamba na hilo aliupongeza mkoa wa Tanga kwa kuendesha maonyesho hayo kiufanisi huku akiitaka mikoa mingine nchini kuiga mfano kwa lengo la kuongeza thamani mazao ya kilimo na utoaji huduma
"Nipende kutoa shukurani kwa viongozi wote walioshiriki kufanikisha maonyesho haya, ni jambo la faraja kwa kushirikiana na serikali hii ya mkoa, nimeambiwa kuna washiriki zaidi ya sabini na nne, kwa makampuni mengine hayajafanikiwa kushiriki kwa tatizo moja au jingine niwaombe sana kadri yatakavyoendelea mshiriki, lengo la serikali ni kuona hatumuachi mtu nyuma" alieleza.
Kigahe aliongeza kuwa lengo la serikali na kuwa na uchumi wa viwanda ambao ni jumuishi kwa ajili ya maendeleo ya watu.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments