Charles James, Michuzi TV
BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia Mei 27 mwaka huu imeidhinisha mikopo mitatu ya masharti nafuu yenye jumla ya Sh Trilioni 2.0125 kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema pia bodi hiyo pia Juni 3 mwaka huu imeidhinisha mkopo mwingine wa Sh Bilioni 326 na kufanya jumla ya mikopo hiyo ya masharti nafuu kufikia minne ikiwa na thamani ya Sh Trilioni 2.3391.
Dk Nchemba amesema miradi iliyopata idhini ya bodi hiyo mradi wa RISE wenye lengo la kuboresha barabara za vijijini ambao umepewa mkopo wa dola za Marekani Milioni 300, mradi wa kusaidia mazingira wa HEET wenye mkopo wa dola milioni 425.
Miradi mingine ni mradi wa DTP wa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao ambao umepewa mkopo wa dola milioni 150 na mradi wa ZESTA wa umeme Visiwani Zanzibar wenye mkopo wa dola milioni 142.
" Hii ni neema kubwa sana kwa Nchi yetu kupewa mikopo ya fedha nyingi kiasi hiki ikiwa na masharti nafuu, Imeonesha jinsi gani Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia ina imani kubwa na Rais wetu wa kihistoria, Mama yetu Samia Suluhu Hassan.
Kuaminiwa na Benki ya Dunia siyo jambo dogo kwa Nchi yetu, sisi wengine hata kuaminiwa na Vicoba au vikundi kupewa mikopo ni shida, tunawashukuru Benki ya Dunia lakini nimpongeze Rais Samia kwa kufanikisha hili," Amesema Dk Nchemba.
KUHUSU TAKWIMU ZA DENI LA TAIFA
Waziri Dk Nchemba amelizungumzia deni la Taifa likijumuisha la sekta binafsi hadi kufikia mwisho wa April mwaka huu lilikua dola milioni 31,986 kati ya deni hilo, deni la nje ni dola milioni 24,477 na deni la ndani ni dola milioni 7,509.
Amesema deni la Serikali ni dola milioni 26,416 sawa na Sh Bilioni 60,719 ikijumuisha deni la nje ni dola milioni 18,907 na deni la ndani ni dola milioni 7,509 sawa na Bilioni 17,259.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments