UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa ulipambana kwa hali na mali kwa ajili ya kuweza kumbakisha kiungo wao Carlos Carlinhos kwa kuwakodi wapishi kutoka ubalozi wa Angola ila mwisho wa siku nyota huyo aliamua kuvunja mkataba.
Mei 31 Yanga ilitoa taarifa rasmi ya kuachana na kiungo huyo raia wa Angola baada ya kuomba kusitishiwa mkataba na ilipitishwa baada ya pande zote mbili kuketi.
Ofisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema:"Ni kweli Carlinhos ameondoka ila uongozi wa Yanga ulifanya kila jitihada kuona kwamba namna gani anaweza kubaki ndani ya Yanga kwa kufanya kila lililohitajika.
"Mwanzoni alipokuja kulikuwa na shida katika chakula ambapo tuliamua kukodi wapishi kutoka ubalozi wa Angola.
"Wapishi wale walikaa kambini kisha baadaye walianza kuwa train (kuwafundisha) wapishi wetu kisha baadaye akasema mkewe aletwe anahitaji chakula kinachopikwa nyumbani, mkewe akaletwa.
"Tulifanya kila jitihada kumfanya abaki ila baadaye tukaona kwamba hakuwa tayari na tukajua kwamba hakuwa tayari kwa kuwa hakuwa na furaha, labda hakuwa ameandaliwa kucheza katika mazingira yote, mchezaji professional anacheza katika hali zote," amesema Bumbuli.
Ndani ya Ligi Kuu Bara, Yanga imecheza jumla ya mechi 29 ina pointi 61 na imetupia jumla ya mabao 43 katika mabao hayo ni sita nyota huyo alihusika ambapo alifunga matatu na kutoa jumla ya pasi tatu za mabao.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments