Wanaodaiwa kuteswa na Sabaya wafunguka | ZamotoHabari.

 


Dar/Arusha. Baadhi ya watu wanaoishi Kilimanjaro na Arusha wanaodai kufanyiwa vitendo vya ukatili na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya wamesimulia magumu waliyopitia kwa kiongozi huyo.


Sabaya ambaye anashikiliwa na vyombo vya dola kwa mahojiano ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili, alisimamishwa kazi na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 13, mwaka huu.


Kabla ya Sabaya hajasimamishwa kazi alikuwa akituhumiwa kuendesha ukatili, kutumia baadhi ya watu kutesa, kuwatisha wafanyabiashara na kuwalizimisha wampe fedha.


Hata hivyo, tuhuma hizo mara kadhaa alizikanusha akidai kuwa zimekuwa zikienezwa na wabaya wake wakiwemo wale waliokuwa hawataki kufuata sheria na taratibu ikiwemo kukwepa kodi.


Aliyeteswa afunguka


Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Hai, Simon Mnyampanda amedai kuwa ni miongoni mwa  

Akizungumza kwa simu na Mwananchi juzi, Mnyampanda alidai kuwa siku hiyo alijikuta mikononi mwa watekaji alipokuwa katika hoteli ya Giraffe alipoitwa na wahudumu wa hoteli hiyo.


Amedai kuwa wahudumu hao walimweleza kuna mgeni mmoja kati ya waliokwenda kwenye msiba wa kaka yake Freeman Mbowe hakuwa amelipia chumba, aliamua kumlipia pesa hiyo kwa sababu alikuwa anamfahamu.


Mnyampanda amedai baada ya mazungumzo hayo, dada mmoja aliingia na kwenda karibu na meza yake na kabla dakika tano hazijaisha, wakaingia vijana wa kiume wawili waliodai kuwa yule dada ni mke wao.


“Mmoja wao akaniuliza wewe umetoka wapi na huyu mke wetu? Wakati huo mmoja wao anasogea karibu yangu. Mimi nikawajibu kuwa huyu dada wala simfahamu. Nilipojibu hivyo nilipigwa kofi kubwa la shingoni, nilipogeuka nikakutana na bastola nikaambiwa niko chini ya ulinzi,” anasimulia.


Amedai kuwa walimchukua wakampeleka chumbani pamoja na yule mwanamke wakaanza kumtesa.


“Nikawauliza mnataka nini? Wakasema kwanza hujamaliza kuvua nguo, hapo nilikuwa nimebakiza bukta. Niliwaza mambo mengi sana huku nikiangalia njia za kujinasua,” alidai.


Katika harakati za kupambana kujiokoa, alimpiga ngumi mmoja wao, jambo lililowaudhi na wakampulizia kemikali machoni ambazo zilimfanya asione kwa muda.


Alidai walipomtoa nje alifanikiwa kuona kundi jingine na na magari matatu waliyopanda na kwenda kwenye barabara ya Arusha Moshi.


Alidai msafara huo uliokuwa ukiongozwa na gari la Sabaya ulipita maeneo ya Kwa Sadala, Mto Kikavu na walikuwa wakimuuliza kama anaona na aliwajibu kuwa haoni. Amedai akiwa ndani ya gari hilo waliendelea kumshambulia.


“Wakawa wanajadiliana mbona tunampiga sana hajibu, au atakuwa amekufa? Na mimi nikajikaza na kujifanya kuwa nimekufa. Mwingine akasema au tummalizie kwa risasi? mwingine akajibu huyo ameshakufa tutapoteza tu risasi, wakasema wanituipe kwenye mto, lakini Sabaya akaja tena na akawaambia sasa huyu tusimtupe mtoni, tukamfanye darasa kwa wenzake kuwa ameingia mwanaume Hai hataki tena Chadema wilayani mwao.”


Amedai kuwa wakati huo alikuwa ameshavunjika miguu yote na mikono huku baadhi ya vidole vikiwa vimesagwa.


“Wakaenda kunitupa huko Hai Day Sekondari karibu na makazi kisha wakatokomea. Baadaye nikaanza kupiga kelele, ilikuwa saa 9 usiku,” anasimulia kada huyo wa Chadema.


Amedai baadaye alikwenda kijana mmoja akamulika na tochi ya simu yake na akamtambua kwa sababu kutoka hapo hadi nyumbani kwake si zaidi ya mita 300. Kijana huyo aliita watu wakampeleka hospitali ambako bado anaendelea na matibabu hadi sasa.


Wengine walioteswa


Akizungumza na Mwananchi, Peter John ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Hai alidai waliwahi kwenda ofisini kwa Sabaya ili wasaidiwe kusaidiwa kutatua mgogoro wa umiliki wa ardhi, lakini akatakiwa atoe fedha na alipotoa kidogo aliishia kuteswa mpaka alipotoa Sh5 milioni.


Mkazi wa Njiro, Ismal Juma alisema alinunua gari kwa kufuata taratibu zote, lakini alijikuta akishindwa kulipwa fedha baada ya kuuza kutokana na Sabaya kumtisha kuwa gari lake lilikuwa ni la wizi.


“Alinipigia simu na kuniambia nimemuuzia mlinzi wake gari la wizi na kama nataka amani nisidai tena malipo yangu,” alidai


Diwani wa Kata ya Sombetini, Jiji la Arusha, Bakari Msangi, akimwelezea Sabaya hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari alidai, alikuwa akifanya ukatili na walinzi wake binafsi sita wanaotembea na silaha.


Diwani Msangi alidai Februari 9, mwaka huu, alipokea simu kutoka kwa mtu mmoja (jina linahifadhiwa) akimweleza kuwa Sabaya amevamia dukani kwake.


Alidai kuwa alipofika dukani alimkuta Sabaya na vijana wake wamewaweka chini ya ulinzi wafanyakazi na wateja waliokuwa kwenye hilo duka, wanawapiga.


Alidai kuwa Sabaya alikuwa anadai mfanyabiashara huyo ni mhujumu uchumi, wanafanya biashara haramu wanauza dola feki, wanauza bidhaa hawatoi risiti.


Tangu kushikiliwa kwa Sabaya, watu mbalimbali wameanza kujitokeza wakimshutumu kwa kuhusika kwenye matukio maovu. Hata hivyo, uchunguzi ulioitishwa na Rais Samia ndio unasubiriwa kwa hamu kubwa kutoa majibu ya tuhuma zote zinazomkabili kama zina ukweli ama vinginevyo wakati huu akiendelea kushikiliwa na vyombo vya dola.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini