Baraza Kuu Chadema Kuamua Hatima Kina Mdee | ZamotoHabari.

 


Dar es Salaam. Mbivu na mbichi kuhusu uanachama ndani ya Chadema kwa wabunge 19 wa viti maalumu utajulikana baadaye mwezi huu, wakati Baraza kuu la chama hicho litakapoketi kujadili rufaa yao waliokata dhidi ya uamuzi wa kamati kuu ya kuwavua uanachama.


Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake l(Bawacha), Grace Tendega (aliyekuwa katibu mkuu wa baraza hilo) Agnesta Lambet (aliyekuwa Mwenezi) na Jesca Kishoa (aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara- Bawacha).


Wengine ni Ester Bulaya, Ester Matiko, Salome Makamba, Nusrat Hanje, Tunza Malapo, Conchestar Rwamlaza, Naghenjwa Kaboyoka, Hawa Mwaifunga, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Asia Mohammed, Sophia Mwakagenda, Cecilia Pareso na Felister Njau.


Kwa pamoja wabunge hao 19 walivuliwa nyadhifa za uongozi pamoja na uanachama kutokana na uamuzi wa kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichoketi Novemba, mwaka jana baada ya kubaini wamekwenda kinyume na msimamo wa Chadema. Hata hivyo licha ya kufukuzwa uanachama, wamekata rufaa katika baraza kuu la chama hicho.


Ingawa hakutaja ajenda ya mkutano wa baraza kuu, lakini jana Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aliwaambia viongozi chama hicho mkoani Mwanza kuwa kikao hicho cha siku tatu kitafanyika baada ya kumalizika kwa ziara ya vikao vya ndani iliyopewa jina la ‘Operesheni Haki’ iliyoanza Mei 25.


Taarifa zilizofikia gazeti hili, ziara hiyo inayofanywa na viongozi wakuu wakiwemo manaibu makatibu wakuu na wenyeviti wa mabaraza ya chama hicho inatarajiwa kuihitimishwa Juni 27 mjini Unguja. Baada ya hapo siku zinazofuatwa huenda kikao hicho cha siku tatu cha baraza kuu kitaketi.


ADVERTISEMENT

“Tukitoka hapa tunakwenda Kanda za Magharibi, Kati, Nyasa, Kusini, Pwani, Pemba kisha tunamalizia Unguja. Tukimaliza mzunguko huu tunakwenda kufanya kikao cha baraza kuu la taifa la chama lenye wajumbe zaidi 600 kutoka maeneo yote nchini.


“Kikao hiki cha siku tatu kitafanyika kwenye kanda itakayofanya vizuri kwenye operesheni haki. Kwa hiyo hii ngoma nawaachia nyie maana Kanda ya Kaskazini, Serengeti, Mbeya na Dar es Salaam wote wanataka kikao hiki kifanyike kwenye maeneo yao,” alisema Mbowe.


Hivi karibuni Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia gazeti hili kuwa kikao hicho kinatarajiwa kuketi mwezi huu kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, akifafanua kuwa pamoja na mambo mengine kitajadili bajeti ya mwaka ya chama hicho.


“Kitajadili pia mpango kazi wa chama wa mwaka, kwa vile wanawake wale 19 walikata rufaa basi itajadiliwa na kutolewa uamuzi kwenye kikao hicho.


“Unaweza kusema kikao cha baraza kuu ndicho kitakachoamua hatima yao kulingana na uamuzi wa wajumbe tusubiri tuone itakavyokuwa,” alisema Mrema.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini