Umoja wa Ulaya umesema zaidi ya nusu ya raia wake watu wazima wamepatiwa chanjo kamili ya Covid-19, wakati nchi barani humo na Asia zikiendelea kukabiliana na maambukizi mapya yanayochangiwa na kirusi cha Delta.
Umoja wa Ulaya umesema watu milioni 200 wamepatiwa chanjo kamili, ikiwa ni nusu ya idadi ya watu wazima, lakini bado wameshindwa kufikia lengo la asilimia 70 hadi majira ya joto.
Kansela Angela Merkel amesema visa vya maambukizi nchini Ujerumani vinapanda kwa kiasi kikubwa. Ujerumani inaungana na nchi nyingine za ulaya, ambazo zimeshuhudia ongezeko la maambukizi ya Covid-19 katika wiki za hivi karibuni yanayochangiwa na kirusi cha Delta kilichogunduliwa mara ya kwanza nchini India.
Benki kuu ya Ulaya imesema wasiwasi juu ya wimbi la maambukizi inamaanisha kuwa milango ya fedha ya uokozi iko wazi ili kuhakikisha kuwa uchumi ambao ulikuwa umeanza kuimarika hauporomoki tena. Mkuu wa benki hiyo Christine Lagarde ameonya kuongezeka kwa wasiwasi wa kiuchumi unaotokana na kirusi cha Delta wakati benki hiyo ikiuweka vizuri mfuko wake wa uokoaji uchumi kufuatia mkutano wa baraza la wanachama wake 25.
EU-Gipfel Brüssel Christine LagardeMkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Christine Lagarde
“Uchumi katika kanda ya sarafu ya euro unaendelea kuimarika vizuri lakini mwelekeo huo unategemea na mwenendo wa janga na maendeleo ya chanjo. Kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa sasa kunatarajiwa kuwa kwa muda mfupi, shinikizo la bei linaweza kupanda polepole, ingawa mfumuko wa bei katika kipindi cha muda wa kati bado uko chini ya malengo yetu. Hatua zetu za kisera zitasaidia uchumi kuimarika kikamilifu na mwishowe kupunguza mfumuko wa bei katika malengo yetu ya asilimia mbili’
Uingereza ambayo iliondoa vizuizi vingi mapema wiki hii nayo imeshuhudia kupanda kwa maambukizi na maduka makubwa nchini humo yalionya juu ya uwezekano wa uhaba wa chakula kwasababu wafanyakazi wengi wamelazimishwa kujitenga. Ufaransa wiki hii ilitangaza masharti mapya yanayotaka kibali cha afya kwa matukio yote au maeneo ya watu zaidi ya 50. Italia nayo imesema jana kuwa vibali vya afya vitakuwa lazima kwa watu wanaotaka kwenda migahawani, kuogelea na maeneo mengine ya burudani.
Nchi katika ukanda wa Asia nazo zimeshuhudia mlipuko mbaya hadi sasa, ambapo Indonesia imekuwa kitovu cha maambukizi ulimwenguni huku Vietnam na Thailand zikikabiliwa na masharti mapya ya kupambana na maambukizi.
Hapo Alhamis mechi moja ya kimataifa ya mchezo wa kriketi baina ya West Indies na Australia jijini London ilifutwa dakika za mwisho kutokana na kugundulika kisa cha Covid-19 miongoni mwa wajumbe wa benchi la timu ya West Indies.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments