Wakulima 2,176 nchini wanufaika na mafunzo stadi za kilimo na ufugaji kupitia mradi wa Tajirika na Kilimo | ZamotoHabari.

Jumla ya wakulima 2,176 (wanawake 1,294 na wanaume 882) wa mikoa ya Morogoro, Iringa na Njombe wamenufaika na mafunzo ya stadi katika kilimo  na ufugaji yaliyotolewa kupitia mradi wa Tajirika na Kilimo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kimataifa la CARE na Taasisi ya Ukuzaji Kilimo Uwanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
 
Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021, Mratibu wa Mradi huo kutoka VETA, Bw. Perecy Ugula, amesema wakulima hao walipatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa mifugo hasa ng’ombe wa maziwa na kuku, kilimo cha mazao mchanganyiko, na kilimo cha mbogamboga na matunda, na kufanikiwa kubadili uendeshaji wa shughuli zao hizo kuwa za kisasa na za kibiashara.
 
Kwa mujibu wa Bw. Ugula, mafanikio mengine yaliyopatikana kwenye mradi huo ni pamoja na uandaaji wa mitaala miwili ya sekta ya Kilimo, ambayo ni Mtaala wa Kilimo cha Mbogamboga na Matunda, Mtaala wa Kilimo cha Mazao, na kuuboresha mtaala wa Afya na Ufugaji wa Mifugo.
 
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Kimataifa la CARE, Bw. Edwin Sallu, amesema kupitia utekelezaji wa mradi huo wamegundua uwepo wa uhitaji mkubwa wa mafunzo ya stadi za kuboresha shughuli za kilimo kwa wakulima wadogowadogo vijijini na kwamba wengi wao wako tayari kugharamia mafunzo hayo kama inavyofanyika sasa katika Mradi wa Tajirika na Kilimo, hivyo akaiomba VETA kupanua zaidi wigo wa mafunzo kwa mfumo wa kuwafuata wahusika katika maeneo yao vijijini.
 
Sallu amesema mafunzo hayo yamewezesha kuunda vikundi 141 vya uzalishaji katika sekta ya kilimo cha mazao mchanganyiko, Mbogamboga na matunda na ufugaji wa kibiashara, ambapo kwa sasa wanafanya shughuli zao za kilimo kwa umoja, hali inayowezesha uzalishaji mazao kwa wingi, ubora na uhakika wa kufikia masoko ya bidhaa zao na kuwezesha wakulima hao kukopesheka kwa urahisi na kupata faida nzuri.
 
“Kwa kweli tumeshuhudia manufaa makubwa ya mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huu kwa wakulima vijijini, hasa ukizingatia kuwa asilimia 67 ya wanufaika ni wanawake na watoto wa kike ambao tunaamini wataleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao,” amesema.
 
Meneja wa Kongani ya Kilombero kutoka Taasisi ya SAGCOT, Bw. John Nakei, amesema kuwa Taasisi yake itaendelea kutoa ushauri, kuwaunganisha na fursa za masoko, na kutoa elimu zaidi kwa wakulima katika mikoa hiyo ili kuwasaidia kuendesha shughuli hizo za kilimo kwa tija zaidi na kuwezesha uzalishaji endelevu wa chakula.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah, licha ya kuwapongeza wadau katika utekelezaji wa mradi huo, ameshauri kuweka mkakati wa uendelezaji wa shughuli zilizofanywa kwenye mradi huo ili wakulima wengi zaidi wanufaike na mafunzo hayo.
 
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za Juu, Bi. Susan Magani, amesema VETA inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia wananchi wengi zaidi, hasa maeneo ya vijijini, na kwamba anaamini kuwa wakulima wengi zaidi nchini watanufaika na mafunzo hayo ili kuboresha shughuli zao.
 
Mradi wa Tajirika na Kilimo ulianza kutekelezwa mwaka 2018 kwa lengo la kujenga na kuimarisha ujuzi katika sekta ya kilimo kwa wakulima 2,200 na  unatarajiwa kumalizika Desemba 2021.

Watekelezaji wa Mradi wa Tajirika na Kilimo katika picha ya pamoja wakati wa  kikao kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Nyanda za Juu, Bi Susan Magani, akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021.
Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Kimataifa la CARE, Bi Haika Mtui,  akiwasilisha mada wakati wa kikao kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021.
Mratibu wa Mradi wa Tajirika na Kilimo kutoka VETA, Bw. Perecy Ugula akiwasilisha mada wakati wa kikao kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah, akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021.
Mratibu wa Mradi wa Tajirika na Kilimo kutoka Shirika la CARE Bw. Samuel Chambi akisisitiza jambo kwa watekelezaji wa Mradi huo wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tajirika na Kilimo kilichofanyika  jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23 Julai 2021
 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini