Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi wa jengo la karakana ya wenye mahitaji maalum mkoani Katavi ambalo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulitoa fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi huo ambao haujakamilika mpaka sasa.
Akizungumza na Viongozi wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi ambao ndio waasisi wa mradi huo, Ndejembi amesema TASAF ilitoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wenye ulemavu mkoani Katavi kujenga karakana hiyo ili waweze kufanya shughuli zao kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Ndejembi amesema watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii, na licha ya kuwa na ulemavu wameonyesha dhamira ya kujishughulisha na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kuungwa mkono na Serikali na jamii kwa ujumla.
Ndejembi ameongeza kuwa, chama hicho cha walemavu kilikuja na wazo la kuanzisha mradi huo ili wajishughulishe na ushonaji na kuwa na ofisi ya kikundi ambayo itaratibu ushiriki wao katika uzalishaji kwa manufaa ya taifa, hivyo atakaa na uongozi wa TASAF ili kuangalia namna ya kuwezesha ukamilishaji wa ujenzi huo baada ya uchuguzi wa TAKUKURU kukamilika.
Naibu Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa TAKUKURU kukamilisha uchunguzi kabla ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo, lengo likiwa ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa awali pamoja na kulinda hadhi ya Mwenge wa Uhuru ambao Kiongozi wake aliweka jiwe la msingi tarehe 20 Septemba, 2012.
Aidha, Ndejembi amezungumzia hoja ya mgogoro wa kiwanja uliowasilishwa na Viongozi wa Chama Cha Walemavu waliodai kiwanja chao kuvamiwa na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph kujiridhisha na mmiliki halali wa kiwanja hicho ili fedha zikipatikana ujenzi uanze mara moja badala ya kuanza kutatua mgogoro.
Naye Katibu wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi, Godfrey Sadala amesema lengo la kujenga karakana hiyo ni kutoa fursa kwa walemavu wengine mkoani humo ili wapate eneo la kujifunza na kuondokana na dhana potofu kuwa mtu akiwa mlemavu hawezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Joshua Sankala amesema mradi huo uliibuliwa kipindi cha pili cha TASAF ili kusaidia watu wenye ulemavu kufanya shughuli zao zitakazowakwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine Ndejembi amewasisitiza walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri Ndejembi amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini ulianzishwa na Serikali kwa lengo kuboresha maisha ya kaya maskini, ndio maana katika Kijiji cha Kawanzige pekee kiasi cha shilingi milioni 118 zimetolewa kwa walengwa badala ya kupelekwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu zoezi la uandikishaji kwa wale ambao hawajaandikishwa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu amesema kipaumbele cha uandikishaji kilitolewa kwenye vijiji ambavyo havikuwahi kuandikishwa kabisa.
Ameongeza kuwa, zoezi la uandikishaji litaendelea kuanzia tarehe 10 mwezi huu, hivyo amewataka ambao hawajaandikishwa kuvuta subira mpaka zoezi hilo litakapoanza.
Ndejembi amewatembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku wanayoipokea kutoka TASAF ili waweze kuboresha maisha yao.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu akitoa ufafanuzi kuhusu uandikishwaji wa walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
Naibu Waziri Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments