Waziri Ndugulile apongeza ubia wa Benki ya CRDB na Shirika la Posta kupitia CRDB Wakala, asema utachochea ujumuishi wa kifedha | ZamotoHabari.

Benki ya CRDB imezindua upya huduma za CRDB wakala kupitia Shirika la Posta Tanzania kwa ajili ya kuwawezesha wateja na Watanzania kwa ujumla kupata huduma za benki hiyo kwa urahisi na unafuu. Hafla ya uzinduzi ilifanyika katika makao makuu ya Posta jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi hizo.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ndungulile alisema kuwa ubia huo wa Benki ya CRDB na Posta utasaidia kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini kwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Aidha alibainisha kuwa Serikali kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano imejipanga kuhakikisha matumizi ya njia mbadala za kutoa huduma za kifedha yanaongezeka ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani waliopo vijijini.
“Nimefurahishwa sana kuona Benki ya CRDB ikiwa mstari wa mbele katika eneo hili, kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma ikiwamo CRDB Wakala. Niwaombe mkasimamie vizuri ubia huu ili huduma zinazotolewa zikawe na manufaa kwa Watanzania wengi,” alisema Waziri Ndungulile.

Waziri Ndungulile aliwataka wananchi kutumia vizuri fursa hiyo ya CRDB Wakala kupitia Shirika la Posta kupata huduma za kibenki hasa ukizingatia kuwa shirika hilo lina ofisi katika kila wilaya nchi nzima.
“Ripoti ya Ujumuishi wa Fedha ya Finscope inayoonyesha ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania wote ambao wanapata huduma za benki. 
 
Tukiitumia fursa hii vizuri tutakwenda kuongeza idadi ya watanzania waliounganishwa katika mfumo rasmi wa kifedha,” alisisitiza huku akizitaka Benki ya CRDB na Shirika la Posta kutoa elimu ya kutosha juu ya huduma hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimweleza Waziri Ndungulile kuwa kupitia ubia huo Benki ya CRDB itatumia ofisi zaidi ya100 za Shirika la Posta kufikisha huduma kwa wateja kutumia mfumo wa CRDB Wakala. 
 
Alisema uzinduzi wa huduma hiyo ni sehemu ya mkakati wa Benki ya CRDB kubuni namna bora ya kufikisha huduma kwa wateja ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuongeza ujumuishi wa kifedha.
 
“Niwakaribishe wateja wetu wote nchi nzima na hata wale wasio wateja kupata huduma zetu kupitia Shirika la Posta kwani huduma zote zinapatikana kupitia madirisha ya CRDB Wakala,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa kupitia ubia huo wateja wataweza kunufaika na huduma nyingi za benki hiyo ikiwamo kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha, kulipia Ankara, kulipa tozo na kodi za Serikali, kulipia bima na huduma nyengine nyingi za kibenki.
Akielezea mafanikio ya CRDB Wakala tokea kuanzishwa kwake mwaka 2013, Nsekela alisema mpaka sasa Benki hiyo ina zaidi ya mawakala 20,000 waliosambaa kote nchini mijini na vijijini. Alibainisha zaidi kuwa mfumo huo umesaidia kupunguza gharama ya kufikisha huduma kwa wateja lakini pia kutoa ajira kwa watanzania na hivyo kukuza kipato cha wananchi. 
 
“Ninajivunia kusema tumepata mafanikio makubwa sana kupitia mfumo huu wa CRDB Wakala, sasa hivi zaidi ya asilimia 40 ya miamala ya wateja hufanyika kupitia CRDB Wakala kulinganisha na matawi,” alisema Nsekela.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Posta, Bwana Macrice Mbodo alimhakikishia Waziri Ndungulile kuwa shirika lake limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha malengo ya ubia huo ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi yanafikiwa.  Alisema ubia huo utakua na manufaa kwetu kwao kwa kuwezesha kupata kamisheni, hivyo kuwa sehemu ya vyanzo vya mapato vya shirika. 

“Tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi. Nikuahidi Mheshimiwa Waziri tutasimamia vizuri utoaji wa huduma kwa wateja ili kuhakikisha wanapata pia kutoa huduma kwa urahisi na haraka,” alisema Mbodo huku akiishukuru Benki ya CRDB kwa mafunzo ambayo wameyatoa kwa wafanyakazi wa shirika ili waweze kutoa huduma kwa weledi wa hali ya juu. 
 
Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa huduma za CRDB Wakala kupitia Shirika la Posta

Mkuu wa Kitengo cha CRDB Wakala, Ericky Willy akiwasilisha mada kuhusu huduma zinazopatikana kupitia madirisha ya CRDB Wakala katika ofisi za Shirika la Posta


Msanii Mrisho Mpoto akitumbuiza wakati wa uzinduzi huo






APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini