JOSEPH HAULE MSANII ANAYEYAISHI ALIYOYAIMBA II | ZamotoHabari




Adeladius Makwega-DODOMA.

Katika sehemu ya kwanza ya matini hii nilikueleza namna muziki huu wa kizazi kipya ulivyoanza na namna Joseph Haule alivyokutana na Afande Sele pale Kingurunyembe sekondari pia nilieleza harakati za muziki huo tangu mwanzo.Siku ya leo naendelea na matini hii.

Msanii mwingine anayefahamika kama Raymond Mahira maarufu kama Bunju Mani alikuwa na kundi hili la Hard Crewz Mob.

“Sisi tulianza muziki huu mapema sana na nilikutana na Modestus walikuwa wakifanya muziki na siku moja wakati huo nyumbani kwetu ilikuwa Mbagala Kipati kama mwaka 1995, kuna siku nilipita wakanisimamisha wakaniuliza ndugu unasoma wapi? Nikawaambia nipo DIT nikawa rafiki yao. Tukawa tunafanya matamasha yanaandaliwa huku shule na shule zikishiriki akiwamo Msafiri Kondo (Solo Thang), Mode Fox, Juma Nature, DERZ Chifu na wengineo.”

Siku moja huyu Nigger Jay aliomba kupanda Jukwani na huyu Modestus akamwambia mbona wewe hatukufahamu? Akaambiwa ebu rapu kidogo, kweli ndugu huyu akaimba baadhi ya mistari mbele yetu.

“Wakati huo Sugu, Solo Thang na Balozi walikuwa na Programu maalumu ya kuibua vipaji mimi nilikuwa mdogo, kwa hiyo walinichukua katika mpango wao wa kuibua vipaji kwa wasanii wadogo. Mshindani mkubwa wa Sugu wakati huo walikuwa na Hard Blasterz ambao ni akina Terry na Big Wile na wakati huo walikuwa na album yao ya Chemsha Bongo.”

Afande Sele anasema kuwa Solo na Sugu wakiwa nayeye na hawa Hard Blasterz walikuwa na Josephy Haule (Niga Jay). Sugu akasema jamani tuna msanii wetu tunayesimamia anatokea huko Morogoro anaitwa Seleimani huku jina la Afande Sele akiwa hajapewa na Sugu akasema bado tunamtafutia jina, tunataka aendeleze huu mziki.

Naye Fanani Terry na Big Wille wakasema tuna kijana wetu lakini anafanya kazi Tanga katika kampuni moja ya simu.

“Kwa hiyo hapo ndipo nilipokutana uso kwa uso na Profesa Jay ndipo tukawatunafanya naye muziki pamoja katika nyimbo kadhaa ikiwamo mtazamo.”

Hard Crewz Mob wanasema kuwa

“Profesa alikuwa akisoma Mbeya walikuwa wakifika katika matamasha hayo, lakini alikuwa akikaa huko Ukonga-Dar es Salaam, huku akiimba na wadogo zake lakini wadogo zake hawa hawakufanya vizuri. Walikuwa wanakuja kuomba katika matamasha yetu, yeye, Judith Wambura (Lady Jay Dee), Sosi B akina Kibacha wa Kwanza Unity hawa sasa wako Ulaya ni kaka zake Sudi Mnette ambaye ni Mtangazaji wa DW Kiswahili.”

Rayomond Mahira anasema kuwa juu ya muziki huu anayo mengi ya kusema na juu ya Profesa Jay hasa akiyatazama maisha ya mwanamuziki huyo yenye mafanikio makubwa.

“Yule Bwana alifanikiwa mno katika muziki wake kutokana na kuweza kujinyenyekeza kwa baadhi ya watu wenye uwezo na nafasi wa wakati huo, ambapo sisi wengine tulikuwa hatuna hicho kipaji, hata mmoja wetu wa Hard Crewz na yeye alifanikiwa kwa mbinu hiyo (Solo Thang). Binafsi ninawapongeza kwa kulibaini hilo ndiyo maana sisi tuliishia hapo hapo, wenzetu wakafika mbali. Hata leo nikikutana na Profesa Jay atanisalimu vizuri akiwambia alionao kuwa mimi ni miongoni mwa wanamuziki wazuri wa wakati huo.”

Kwa upande wake Mtayarishaji P-Funk anasema kuwa Profesa Jay ameweza kurekodi kwake nyimbo nyingi ambazo zote kwa pamoja zimeweza kupendwa sana na wapenzi wake na anasema kuwa ndugu huyu huwa akiamua jambo hulifanya kwa moyo wake wote bila ya kurudi nyuma.

Profesa Jay ni mwanamuzi ambaye aliweza kuingia katika siasa kuingia kwake katika siasa ilikuwa ni hatua ya kuyatenda kwa vitendo yale aliyokuwa akiyaimba katika nyimbo zake. Ulikuwa ni wakati wa wa kuyachukua maudhui yake ya miaka kadha na kuyaweka kwa vitendo.

Mathalani wimbo wa Ndiyo Mzee, Kikao cha Dharura, Bongo Dar es Salaam na nyingine nyingi.

Akiwa mbunge wa Mikumi kati ya mwaka 2015-2020 chini ya serikali Rais wa Awamu ya Tano John Magufuli, Profesa Jay aliweza kuinua sauti yake na kuwasemea Watanzania wengi.

“Mimi naitwa Josephy Leornad Haule Mbunge wa Mikumi ninayaeongoza Binadamu na Wanyama, mheshimiwa rais hapa Mikumi tuna tatizo la maji tunataabika sana, lakini pia mheshimiwa rais Barabara kutoka Korogwe mpaka Handeni inapitia Turiani inakuja inapita Dumila inapita Kilosa inakuja Mikumi inakwenda Malinyi na mwisho inatokea Songea bado hatujapata muelekeo kama ulivyoahidi katika ahadi zako, tunaomba ikamilike.”

Haya yote alielezwa Rais Magufuli akiwa Jimboni Mikumi na enzi za Mbunge Josephy Haule.
Mpaka leo sifahamu kama yamefanyiwa kazi au la, kwani si madhumuni ya makala haya kwa leo.
Swali ni je Joseph Haule alifanikiwa katika kipindi chake cha siasa cha miaka mitano kama mbunge?

Kama ndiyo katika lipi na kama hapana kwa nini?

Binafsi sina kipimo cha kuyapima hayo.

Kubwa la kusema ni kuwa Profesa Jay alitimiza wajibu wake kama mbunge wa wakati huo kwa kuwasemea wapiga kura wake kama ulivyosikia juu ya kero ya maji na barabara alivyoitaja ya kuunganisha Korogwe na Songea.

Msafiri Kondo, Ulamaa (Solo Thang) ambaye ni miongoni mwa wasanii wa Hard Crewz Mob huku akitajwa na wengi katika maisha ya Profesa Jay anakumbuka sana namna walivyokutana na Josephy Haule miaka mingi na anakumbuka namna walivyoshirikiana naye kufanya muziki huo.

“Huyu ni ndugu yangu, huyu ni kaka yangu na huyu ni msanii mwezangu naweza kusema kuwa Joseph Haule n msanii anayeyaishi aliyoyaimba.”

Binafsi ninayeandika matini hii kama nilivyoeleza kuwa nilikua miongoni mwa wanaoupinga muziki huo kutokana na mazingira ya awali nilivyoyashuhudia kwa macho yangu nakumbuka niliwahi kushuhudia tamasha moja la Joseph Haule mwaka 2002 ambapo alifika Chuo cha Ualimu Kasulu, miongni mwa watu waliompokea akiwamo ni Hija Mashaka na Seralini Sawa ambao walikuwa viongozi wa wanachuo hiki wanaojihusisha na burudani chuoni hapo wakati huo huku na mimi nikiwa pamoja nao.

“Tulimfuata katika nyumba ya wageni aliyofikia ndugu huyu, aliponiona alinifananisha na rafiki yake Modestus Makwega (Mode Fox wa Hard Crewz Mob) na nilimwambia mimi siyo, yule ni mdogo wangu. Alifika Chuoni Kasulu alitumbuiza katika ukumbi wa chuo hicho akiwa na Fanani Terry na baadaye kuondoka zao” Hii nakumbuka.

Mwanakwetu huyo ndiye Nigga J, Profesa Jay na Joseph Leonard Haule miongoni mwa wanamuziki walioweza kuutangaza muziki wa kizazi kipya kama nilivyojaribu kupita kwa wale waliwahi kukutane naye tangu mwaka 1990 hadi leo.

Makala haya kwa leo yanamtakia siha njema na maisha marefu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257









Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini