WIZARA YETU MALI YA WATANZANIA-GEKUL | ZamotoHabari


Adeladius Makwega –WUSM ARUSHA


Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Bi Pauline Gekul Machi 29, 2022 akiwa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Waigizaji wa Filamu Tanzania Jijini Arusha amesema kuwa wizara yake ni mali ya Watanzania na watendaji wake wanapaswa kufanya kazi kwa kuwasaidia Watanzania wote bila ya ubaguzi.

“Hilo ninatoa ahadi kwenu kama kuna jambo ambalo limekwamishwa litakamilika mara moja na ninatoa siku saba likamilike, kwani watendaji wote wizarani na kwenye taasisis zetu wanapaswa kushirikiana na wadau wote ambao ni nyinyi, hiyo ndiyo azma yangu na Waziri wangu mheshimiwa Mohamed Mchengerwa.”

Naibu Waziri Gekul aliwapongeza waigizaji wa filamu nchini kuendelea kufanya kazi kwa umoja, upendo na kujitokeza katika mikutano yote kwa ya chama hiki kwa wingi kwani serikali tangu wakati wa kupambana na Nduli Iddi Amin wasanii walishiriki vizuri na hata wakati wa kupambana na janga la UVIKO 19 wasanii wamefanya kazi kubwa sana kuielimisha jamii ya Watanzania.

Kuhusu Ombi la waigizaji hao kumualika Rais Samia kushiriki kongamano kubwa la waigizaji nchini Naibu Waziri Gekul amesema atalifikisha na ana uhakika Mheshimiwa Rais atakubali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania Chiki Mchomwa alisema kuwa uigizaji ni rasimali muhimu sana na Tanzania ina waigizaji wengi na kama mipango ikikaa vizuri inaweza kutoa ajira nyingi kwani sanaa ajira zake haina ubaguzi wa rika.

“Tukifanya kazi zetu vizuri tutakuwa tumemsaidia mno Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ni muigizaji mwenzetu, tunamshukuru sana yeye pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuwa pamoja nasi nyakati zote.”

Awali kabla ya hafla hiyo ya ufunguzi, Chama cha Waigizaji Tanzania kilifanya Mkutano wake Mkuu na kiliamua mambo kadhaa likiwamo kuwa na mkutano mkuu wa mwaka mara moja, badala ya mara mbili na kuwapa nafasi wajumbe kadhaa kuingia katika mkutano huo, hayo yakiwa ni mabadiliko makubwa ya katiba ya chama hicho.

Sambamba na hilo mkutano huo uliamua kwa kauli moja kuwa kila mwanachama sasa atalipa Tsh 15,000/- kama ada ya uanachama, kukipa nguvu chama hicho.

Katika hafla hiyo Naibu Waziri Gekul aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Maendeleo ya Sanaa nchini Bi Leah Kihimbi na maafisa wengine kadhaa wizara na taasisi zake.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini