Tangazeni Utamaduni wa Tanzania- Gekul | ZamotoHabari

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewataka watanzania wanaopata furasa za masomo nje ya nchi kuitumia fursa hiyo vyema kuzitangaza tamaduni za Tanzania huko ughaibuni.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul wakati wa maadhimisho ya siku ya Utamaduni wa Baraza la Mahusisano ya Kitamadunina la India (ICCR) iliyoadhimishwa Aprili 09, 2022 katika ubalozi wa India hapa nchini.

Katika maadhimisho hayo yaliyowakutanisha zaidi ya wahitimu 50 walionufaika na fursa za udhamini wa masomo ya elimu ya juu nchini India Mhe. Gekul amesema Serikali inawategemea sana watanzania wanaopata fursa za udhamini wa masomo nje ya nchi kuwa mabalozi wa utamaduni wa nchi yao.

“Mimi ninaamini mnapokuwa huko ughaibuni hamuishii tu kujifunza tamaduni za kwao, bali pia na nyinyi muwafundishe tamaduni zetu, na hasa lugha yetu ya Kiswahili”. Alisema Naibu Waziri Gekul .

Aliongeza kuwa “ tunategemea huko mliko mtakuwa mabalozi wazuri wa kuanzisha vituo vya utamaduni, na madarasa ya kufundishia lugha ya Kiswahili, ili hawa wenzetu wanaotupa ushirikiano na kutufadhili kwenye masomo waweze kujua lugha pamoja na tamaduni zetu”

Halikadhalika amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia na India zimekuwa na mahusiano ya karibu sana kwa miaka mingi sasa na kupitia udugu huo, nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika mambo mbalimbali hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Utamduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaendelea na hatua za utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Kiutamduni kati ya India na Tanzania ili nchi hizi mbili ziendelee kunufaika na programu ya ushirikiano katika masuala ya Kiutamaduni.

Kwa upande wake Balozi wa India hapa Nchini Mhe. Binaya Pradhan, Amesema tangu kuanza kwa kwa program hii ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa vijana wa Kitanzania zaidi ya watanzania mia tatu wamenufaika ambapo kwa msimu wa mwaka 2021 – 2022 watanzania 53 wamepata ufadhili katika ngazi za Shahada ya kwanza, Shahada ya Umahiri na Shahada ya Uzamivu.

Katika maadhimisho hayo naibu Waziri Gekul aliambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Nchini, Dkt. Emanuel Temu pamoja na Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Andrian Nyangamale.





 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini