YANGA SC ILEEEE…NUSU FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO (ASFC) | ZamotoHabari


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

YOUNG AFRICANS SC rasmi imefuzu Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa changamoto ya mikwaju ya Penalti 7-6 dhidi ya Geita Gold FC kwenye mchezo wa Robo Fainali uliochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliokuwa wa ushindani dakika zote 90, Geita Gold FC waliimudu Young Africans SC ikiwa kuidhibiti vilivyo safu ya ushambuliaji iliyokuwa na Mshambuliaji mahiri Fiston Mayele. Geita walipata bao la kuongoza dakika ya 86 ya mchezo kupitia kwa Mchezaji wake Offen Chikola baada ya kupokea pasi safi ya Juma Mahadhi.

Dakika ya 90, ndani ya dakika za nyongeza, Young Africans SC walisawazisha bao hilo kupitia kwa Beki wake wa kulia, Djuma Shabani baada ya kutumbukiza wavuni mkwaju wa Penalti, baada ya Beki wa Geita Gold FC, Amos Charles Kadikilo kuunawa mpira ndani ya Penalti boksi.

Mchezo ulilazimika kwenda kwenye mikwaju ya Penalti, ambapo piga nikupige ilifikia mikwaju Sita bila hata timu moja kukosa. Penalti ya Saba, Golikipa wa Yanga SC, Djigui Diarra alikosa Penalti hiyo baada ya kuitoa nje ya lango, haikuishia hapo, Geita FC nao walikosa mkwaju huo wa Saba uliopigwa na Maka Edward.

Mkwaju wa Nane, Yanga SC walipata kupitia kwa Beki wake, Dickson Job huku mkwaju wa Penalti wa mwisho ambao uliizamisha Geita Gold FC ulipigwa na Juma Mahadhi na timu hiyo kuondolewa kwenye Michuano ya ASFC.

Young Africans SC sasa wanawasubiri mshindi kati ya Simba SC na Pamba FC ya Mwanza katika Nusu Fainali ya Michuano hiyo ya ASFC ambapo mshindi anawakilisha nchi kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup).

Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Golikipa wa timu hiyo, Djigui Diarra baada ya kuokoa mkwaju wa Penalti wa mwisho ambao uliipeleka Yanga SC kwenye hatua ya Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC).



Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini