KOCHA MAKATA AFUNGIWA MIAKA MITANO | ZamotoHabari


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

KOCHA Mkuu wa Mbeya Kwanza FC ya Mbeya, Mbwana Makata amefungiwa kujihusisha na Soka kwa kipindi cha miaka mitano sanjari na Meneja wa timu hiyo, David Naftali wakidaiwa kuamuru Wachezaji wa timu hiyo kugomea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC, mchezo uliotakiwa kuchezwa kwenye dimba la Ilulu, mkoani Lindi.

Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kwa kuzingatia Kanuni ya 32:7 ya Ligi Kuu kuhusu kuvuruga mchezo, Kamati hiyo ilikaa Mei 16, 2022 kupitia masuala mbalimbali ya Ligi hiyo.

Hata hivyo, Kamati imeipa timu ya Namungo FC alama tatu na mabao matatu, baada ya timu ya Mbeya Kwanza kudaiwa kutenda kosa la kikanuni la kugomea mchezo wao dhidi ya Namungo FC katika dimba la Ilulu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 17:42 ambayo inaelekeza, mchezo unaweza kuchelewa kwa dakika 30 kama timu itachelewa kufika Uwanjani au kutotimizwa taratibu za mchezo husika.

Mbeya Kwanza FC imedaiwa kugomea mchezo kwa kudai kutokuwepo Gari la kubebea Wagonjwa (Ambulance) katika uwanja huo wa Ilulu, Lindi. Hata hivyo, imedaiwa ‘Ambulance’ ilikuwepo katika uwanja huo, lakini kutokana na uwepo wa mgonjwa wa dharura, Gari ililazimika kubeba mgonjwa huyo na kumpeleka Hospitali kwa matibabu zaidi.

Pia imeelezwa kuwa kulikuwa na Gari aina ya Toyota Prado lenye Namba za Usajili T 297 BCN, ambayo ingetumika kubebea Mgojwa wa dharura endapo angekuwepo katika mchezo huo.

Taarifa ya Bodi ya Ligi imeeleza kuwa Gari hiyo aina ya ‘Ambulance’ ilirejea uwanjani hapo majira ya Saa 10:23 Jioni, licha ya hivyo mchezo huo haukuanza kutokana na kudaiwa kuwepo mgomo huo wa Mbeya Kwanza FC ulioshinikizwa na Kocha Makata na Meneja Naftali.




Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini