Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KOCHA Mkuu wa Mbeya Kwanza FC, Mbwana Makata na Meneja wa timu hiyo, David Naftali wameomba radhi kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB), Wadhamini wa Ligi hiyo na Wadau wengine wa Soka baada ya kupewa adhabu ya kufungiwa miaka mitano.
Kocha Makata na Meneja Naftali walipewa adhabu hiyo ya kufungiwa miaka mitano wakituhumiwa kuamuru Wachezaji wa timu hiyo kugomea mchezo wao wa Ligi ya Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC kwenye uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, Mei 13, 2022.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kocha Makata ameomba radhi kwa TFF, Bodi ya Ligi na Wadau wengine wa Soka kutokana kuonyesha dosari kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa sasa ni miongoni mwa Ligi bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Sisi tusiwe miongoni mwa watu ambao wanaitia doa Ligi yetu ya Tanzania Bara, tunasema Ligi yetu ni Ligi Bora, ubora ambao unachagizwa na Uongozi wa TFF, chini ya Wallace Karia, na Uongozi wa Bodi ya Ligi chini ya Mwenyekiti Steven Mguto na Wadhamini wote,” Makata amesema.
“Toka nimeanza kucheza Soka hadi sasa nimekuwa Kocha, sijawahi kupewa adhabu kama hii, tunaahidi kutakuwa mfano mzuri kwa faida ya Soka letu la Tanzania endapo tutasamehewa adhabu hii”, ameeleza.
Hata hivyo, baada ya kuomba radhi Kocha Makata ameomba Kamati hiyo iliyotoa adhabu kurudia upya hukumu hiyo, amesema kipindi cha nyuma hawakuwa na rekodi mbaya.
Naye, Meneja wa timu hiyo, David Naftali ameomba radhi kwa TFF, Bodi ya Ligi, Wadhamini wa Ligi hiyo sanjari na Wadau wengine wa Soka la Tanzania kwa kitendo hicho kilichopelekea kufungiwa miaka mitano.
Kocha Mbwana Makata na Meneja David Naftali walifungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kwa kuzingatia Kanuni ya 32:7 ya Ligi Kuu kuhusu kuvuruga mchezo, baada ya Kamati hiyo kukaa Mei 16, 2022 kupitia masuala mbalimbali ya Ligi hiyo.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments