Juzi, Jumatano 21, 2022 tulitoa taarifa ya awali kupitia akaunti za mitanao ya kijamii ya Msemaji wa sekta ya Habari na Uchukuzi wa ACT Wazalendo Ndg. Ally Saleh kwa kutoa pole kwa wananchi waliopata ajali ya Treni iliyotokea siku hiyo katika eneo la Malolo Mkoani Tabora.
Ajali hiyo ilihusisha treni iliyokuwa ikifanya safari kati ya Kigoma na Dar es Salaam na chanzo chake kikielezwa ni kuwa hitilafu za miundombinu ya reli kutokana na uchakavu. Treni iliyopata ajali iliondoka stesheni ya Kigoma saa mbili usiku Jumanne Juni 21, 2022 kuelekea Dar es Salaam ikiwa na behewa nane zilizobeba abiria 930.
ACT Wazalendo pamoja na mambo mengine kwenye suala hili tumeona Takwimu za waathirika wa ajali hii zimekuwa na mkanganyiko mkubwa kati ya taarifa kutoka Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Shirika la Reli, Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Wahudumu wa Hospitali ya Kitete. Vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa ajali hiyo imesababisha vifo vya watu wanne (4) na majeruhi wapatao 205.
Aidha, chanzo cha ajali hii haikijawekwa wazi na kutolewa maelezo ya kutosha na mapendekezo ya namna ya kukomesha tena kutokea kwa ajali kwa wakati mwingine. Tunafahamu umuhimu na mchango wa Usafiri wa reli nchini hususani kwenye Mikoa ambayo reli hii inahudumia kama vile Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyinga, Mwanza na Kigoma kwa upande wa reli ya kati.
Shirika la Reli, linasimamia Miundombinu ya Reli na uendeshaji mzima wa usafirishaji wa mizigo na watu kupitia usafiri huu, hivyo ilitarajiwa kuona shirika linashtushwa na kuguswa zaidi kutokea kwa ajali ambayo imeleta athari kubwa kwa wananchi kwa kutoa maelezo ya kutosha na hatua Madhubuti zitakazo rejesha Imani ya wananchi kuhusu usafiri huu.
Kinyume chake, Shirika la reli halijaipa uzito na kutoa hatua madhubuti za kushughulikia waathirika, kutoa taarifa za aendeleo yao, uchunguzi wa chanzo halisi cha ajali na kuimarisha kwa Miundombinu na nyenzo za usafiri wa reli. Kama tulivyotangulia kusema awali; taarifa yetu ya mwanzo ilikusudia kutoa pole, hivyo kutokana na taarifa ya sasa,
ACT Wazalendo tunatoa mapendekezo yafuatayo ili kushughulikia waathirika na kuimarisha uendeshaji wa huduma ya reli nchini:
i. Serikali isiwe inaficha takwimu halisi zinapotokea ajali kama hizi ili kuondoa mkanganyiko na kujulisha umma ukubwa wa ajali.
ii. Serikali ilisimamie Shirika la Reli kuhakikisha kuongezeka kwa ubora wa huduma na usalama wa usafiri huo usioweza kukwepeka na wananchi wengi.
iii. Abiria wote waliojeruhiwa wapatiwe matibabu bure kadri ambayo watayahitaji ili wapone kabisa na warudi katika kazi na maisha yao ya kawaida.
iv. Serikali iandae utaratibu wa kutoa fidia kwa majeruhi watakao pata ulemavu wa kudumu na fidia kwa familia kwa wale waliopoteza maisha kutokana na ajali hii.
v. Uchunguzi wa tukio hilo ufanywe kwa haraka na uweledi ili taarifa sahihi itolewe kwa umma.
Imetolewa na; Ndugu Ally Saleh
asaleh@actwazalendo.or.tz
Msemaji wa Sekta ya Habari, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi ACT Wazalendo
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments