Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SHIRIKISHO la Soka barani Afrika (CAF) limesema kuwa bingwa wa Michuano ya ‘CAF Africa Super League’ anatarajiwa kubeba kitita cha Dola za Kimarekani Milioni 11.5 ambayo ni sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 25 za Kitanzania, kwenye Michuano hiyo ya ngazi ya Klabu ambayo itaanza Agosti, 2023.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Kawaida wa 44 wa Shirikisho hilo uliofanyika jijini Arusha, nchini Tanzania, Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe amesema kiasi cha fedha, Dola za Kimarekani (USD 100 Million) kitatolewa kwa ajili ya mashindano hayo, huku Mshindi akiondoka na zawadi hiyo (USD 11.5 Million).
“Tulitangaza Julai 3, 2022 kwamba jumla ya kiasi cha fedha kitakachowekwa ni USD 100 million katika mashindano hayo, na Mshindi ataondoka na kiasi cha USD 11.5 million”, amesema Dkt. Motsepe kupitia hotuba yake katika Mkutano huo.
“Tunatarajia kutoa kiasi cha USD 1 Million kwa kila nchi Mwanachama wa CAF, kila mwaka kutoka kwenye Mfuko wa CAF Africa Super League. Pia CAF tunatarajia kugawa kiasi cha USD 50 Million kuchangia maendeleo ya Soka la Vijana na Wanawake na mashindano mengine ili Afrika kuwa na ushindani ulimwenguni”, ameeleza Dkt. Motsepe.
Hata hivyo, Dkt. Motsepe amesema wameongeza zawadi kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka USD 12.5 million hadi USD 17.6 million, na maboresho kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kutoka USD 6.375 million hadi USD 9.9 million. Pia, kuongeza zawadi ya ofa kwenye Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yaliyofanyika nchini Cameroon kutoka USD 24.8 million hadi USD 26.650 million.
Dkt. Motsepe amesema Taasisi yake ya ‘Motsepe Foundation’ itachangia USD 10 Million kuendeleza Miundombinu ya Soka na vitu vingine katika elimu kwa Shule zitakazoshinda mashindano ya CAF ya Mabingwa wa Shule za Afrika (CAF Africa Schools Football Championship). Pia CAF imealika Wadhamini wengine wanaotaka kudhamini mashindano hayo kwa maendeleo ya Soka la Afrika.
CAF imeahidi kuhakikisha kuwekeza zaidi katika matangazo ya Runinga na Maudhui bora ili kuhakikisha matangazo ya mpira wa miguu yanaonekana vizuri kwa wadau wote wa Soka la Afrika na ulimwenguni.
Chanzo | CAF
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments