Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KLABU nne za Tanzania zinazoshiriki Michuano ya Kimataifa zinatarajiwa kujitupa viwanjani Septemba na Oktoba mwaka huu kuanza kinyang’anyiro cha kulisaka taji la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) na taji la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).
Timu hizo nne zinazowakilisha nchi Kimataifa ni Young Africans SC, Simba SC ambao wanacheza Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Geita Gold FC, Azam FC ambao wanacheza Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Young Africans SC wamepangwa kucheza raundi ya awali na Zalan FC ya Sudan Kusini, wakati mshindi wa mchezo huo atacheza raundi ya kwanza na kati ya St. George SC ya Ethiopia au Al Ahli Tripoli ya Libya.
Makamu Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC amepangwa kucheza dhidi ya Big Bullets ya Malawi kwenye raundi ya awali, huku mshindi wa kati ya Red Arrows ya Zambia dhidi ya C.D. Primeiro de Agosto
ya Angola atacheza na mshindi kati ya Simba SC au Big Bullets kwenye raundi ya kwanza ya Michuano hiyo ya CAF FL.
Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Wawakilishi wa Tanzania, Azam FC wao watasubiri kwenye raundi ya kwanza, mshindi kati ya Al Akhdar SC ya Libya dhidi ya Al Ahli Khartoum ya Sudan huku wawakilishi wengine wa Tanzania, Geita Gold FC wakicheza dhidi ya Hilal Alsahil SC ya Sudan, mshindi atacheza dhidi ya Pyramids FC ya Misri.
Raundi ya awali inatarajiwa kuanza Septemba 9-11 kwa michezo ya mkondo wa kwanza na Septemba 16-18, 2022 kwa michezo ya mkondo wa pili, huku raundi ya kwanza ikianza kuchezwa Oktoba 7-9, 2022 kwa michezo ya mkondo wa kwanza na Oktoba 14-16, 2022 kwa michezo ya mkondo wa pili, nyumbani na ugenini.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments