KMC FC YAINGIA KAMBINI KUJIWINDA DHIDI YA NAMUNGO | ZamotoHabari



Wachezaji wa Timu ya KMC FC leo wameanza maandalizi kuelekea katika mchezo unaofuata wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaopigwa Oktoba mosi mwaka huu katika uwanja wa Majaliwa Ruangwa Mkoani Lindi.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana imeanza kujifua ikiwa ni baada ya kurejea kambini jana jioni ilipokuwa kwenye mapumziko ya siku mbili tangu ilipocheza mchezo dhidi ya Timu ya Ihefu Septemba 20 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ambapo KMC FC iliibuka na ushindi wa magoli mawili kwa moja.

KMC FC kwa sasa inajiandaa na mchezo huo dhidi ya Namungo badala ya Mtibwa Sugar ambapo awali ulipangwa kuchezwa Septemba 27 kwa mujibu wa ratiba ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutokana na kubadilika kwa ratiba ambapo Septemba 21 ilitoa taarifa ya mabadiliko ya mchezo huo huku sababu ikielezwa kuwa baadhi ya timu zinazohusika kwenye michezo hiyo wachezaji wao wapo kwenye majukumu ya Timu ya Taifa.

“Tulipokea taarifa ya mabadiliko ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao awali ilikuwa tucheze siku ya Jumanne ya Septemba 27 kwenye uwanja wetu wa Uhuru, kwa hiyo hivi sasa tunajiandaa kwa mchezo mwingine ambao tutakuwa ugenini dhidi ya Namungo Oktoba moja kule Ruangwa, hivyo tunajipanga vizuri kutafuta alama tatu muhimu ugenini.

“Wachezaji wote wamesharejea kambini baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili ambayo tulitoa siku tuliyocheza mechi na Ihefu, na wote wamerejea salama wakiwa na nguvu, Afya njema, hari na morali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maandalizi bora ambayo yatatupa matokeo chana kwenye mchezo huo licha ya kwamba tunafahamu fika hautakuwa mwepesi.

Hadi sasa KMC FC imecheza mechi Nne ambapo kati ya hizo tatu ikiwa ugenini huku mmoja ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, kati ya hizo imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Ihefu na kusare michezo miwili ambayo ni dhidi ya Simba pamoja na Polisi Tanzania huku ikipoteza dhidi ya Coast Union.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, KMC ipo kwenye nafasi ya nane ikiwa na jumla ya alama tano, magoli ya kufunga sita na magoli ya kufungwa sita na kwamba inazidi kujiimarisha zaidi kwenye michezo inayokuja ili kuhakikisha kuwa inapata matokeo kwenye michezo inayokuja.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini