WAZIRI MCHENGERWA AIPONGEZA SIMBA KWA KUENDELEZA USHINDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA | ZamotoHabari


Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameipongeza Timu ya Simba kwa kushinda kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imeshinda mabao 2-0 dhidi ya timu Nyasa Big Bullet ya Malawi katika mchezo wa marudiani uliochezwa leo Septemba 18, 2022 kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa ameambatana na Naibu Spika Mhe. Iddi Zungu, Katibu Mkuu wa Wizara yake Dkt. Hassan Abbasi na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Amesema watanzania na wanachama wa Simba wanafurahi kuona wanafanya vizuri katika mashindano haya ambapo amefafanua kuwa Mhe. Rais pia anaipongeza timu hiyo.

Ameongeza kuwa timu hiyo imeonyesha uzalendo ambao unapaswa kuendelezwa ili kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Ameitaka timu hiyo kutoridhika na ushindi walioupata leo na badala yake iendelee kufanya mazoezi zaidi ili kujinoa hatimaye timu hiyo iingie fainali na kuweza kurejesha kombe nyumbani.

"Ninatoa wito kwa timu yetu kutobweteka na ushindi tulioupata leo, watanzania wanakiu ya ubingwa wa kombe hili. Tunahitaji kujituma na kutanguliza uzalendo ili tuwape raha watanzania". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kufanya uwekezaji katika michezo ili kuwasaidia wananchi kueluka na magonjwa hivyo kujenga afya zao.

Kapteni wa timu ya Simba John Boko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwenye michezo.










Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini