TAMISEMI QUEENS, KVZ hazishikiki Ligi kuu Netiboli | ZamotoHabari

Na Peter Stephen, Morogoro
MABINGWA watetezi wa kombe la Ligi kuu ya Muungano ya Netiboli, TAMISEMI QUEENS, na timu ya KVZ kutoka Zanzibar zimekuwa tishio katika michuano hiyo baada ya kushinda michezo dhidi ya wapinzani wao katika ligi kuu ya Netiboli inayoendelea katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

TAMISEMI QUEENS walianza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuifunga timu ya netiboli ya Zimamoto kwa magoli 43-29, na katika mchezo wao wa pili dhidi ya JKU waliichabanga kwa magoli 52-43 na katika mechi yao dhidi ya timu ya Warriors waliifunga kwa jumla ya magoli 70-29.

Nayo timu ya KVZ kutoka Zanzibar ilianza mashindano hayo kwa kishindo baada ya kuifunga timu ngumu ya JKT Mbweni kutoka jijini Dar es salaam kwa magoli 36-35.

Matokeo mengine ya mashindano hayo yaliyoanza juzi hapa mjini Morogoro yanaonyesha kuwa Mafunzo imeifunga Nyika Queens magoli 41-38, Magereza Tanzania imeichapa Warriors magoli 49-32, na Zimamoto imeifunga timu ya Chuo Kikuu cha Kampala magoli 49-45.

Kwa mujibu wa Bi Grace Ilumba ambaye ni Mkuu wa waamuzi, mashindano hayo ya ligi kuu ya Netiboli Tanzania yanashirikisha timu tano kutoka Tanzania Bara na timu tano kutoka Zanzibar.

Bi. Ilumba alizitaja timu hizo kuwa ni TAMISEMI Queens, JKT Mbweni, Magereza Tanzania, Chuo Kikuu Kampala, na Nyika Queens kutoka Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar vinawakilishwa na timu za netiboli za KVZ, JKU, Zimamoto, Warriors na Mafunzo.

Akizungumza mara baada ya mchezo baina ya TAMISEMI Queens na Warriors uliochezwa mapema jana asubuhi nahodha wa TAMISEMI Queens Dafrosa Luhwago ametamba kuwa timu yake italichukua tena kombe hilo mwaka huu na kuahidi kushinda michezo yake yote iliyosalia.

Ameongeza licha ya ligi ya mwaka huu kuwa ngumu anaamini timu yake itashinda kombe hilo kwani imejiandaa vizuri na pia inajivunia kuwa na wachezaji watano wanaounda timu ya Taifa ya Netiboli.

Mashindano hayo yanayoendeshwa kwa mtindo wa ligi yalitarajia kuendelea tena jana jioni kwa michezo miwili na asubuhi ilichezwa michezo miwili.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini