WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa ameipongeza Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) kwa kutafsiri vyema maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo katika sekta ya mchezo na kuwataka kuipeleka program ya Mpira Fursa visiwani Zanzibar ili kuwaandaa vijana watakaolipekeka Taifa katika mashindano ya kimataifa.
Mchengerwa ameyasema hayo wakati akifunga program ya Mpira Fursa inayosimamiwa na kutekelezwa na KTO hafla iliyokwenda sambamba na utoaji wa vifaa vya mchezo kwa vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi na shule za Msingi 86 zilizofikwa na program hiyo ya kuendeleza vipaji kupitia mpira wa miguu.
‘’Kwa dhati niwapongeze KTO kwa kutafsiri vyema ni nini Rais Samia Suluhu Hassan anataka kufanya kwa Watanzania hususani katika sekta ya michezo, jitihada hizi nzuri zinatakiwa kuungwa mkono ili kuipeleka sekta hii ya michezo mbele zaidi hasa katika michuano ya kimataifa ambayo jitihada za Serikali na wadau zimeonekana kwa timu zetu za Taifa kufika katika hatua nzuri ya michuano ya kombe la dunia.’’ Amesema.
Amesema, Uwepo wa Vyuo vya Maendeleo nchini kote ni ukombozi kwa watanzania hasa kwa vijana wa kupata elimu, stadi za maisha, ujasiriamali na fursa ya mpira na kuwataka watanzania kucheza mpira kila Mtaa na Wizara itapokea majina ya vijana wanafanya vizuri kupitia maafisa michezo kama walivyoelekezwa.’’ Amesema.
Pia amesema vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere miaka 1960 nchi nzima vililenga kuleta maendeleo kwa watanzania kupitia elimu na mafunzo ambayo bado yanaasisiwa na Serikali na wadau (KTO,) kwa manufaa ya watanzania.
‘’Licha ya vijana kupata mafunzo katika vyuo hivi pia hupata mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha na kupitia program hii ya Mpira Fursa inayotekelezwa na KTO kwa vitendo ni fursa kubwa…Wakati ni sasa vijana na watoto chezeni mpira Mtaa kwa Mtaa soka inalipa na itasaida kuboresha sekta nyingine…watu tukifanya mazoezi magonjwa yasiyoambukiza yatapungua na kuimarisha sekta ya afya…’’Amesema.
Kuhusiana na ucheleweshwaji wa majibu ya maombi ya usajili wa vyama vya michezo Waziri Mchengerwa amelipa muda wa mwezi mmoja Baraza la Michezo Tanzania (BMT,) kuhakikisha wanakuwa na mfumo wa usajili wa kieletroniki utakaosaidia kupunguza kero kwa watumiaji.
Aidha ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo ambayo kwa sasa kodi kwa baadhi ya vifaa vya michezo imeshuka na kuondolewa na kueleza kuwa kwa miaka 8 kuanzia sasa wamejipanga katika kutekeleza mpango mkakati wa kuhakikisha Tanzania inashiriki katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2030.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO,) Maggid Mjengwa amesema kuwa Taasisi hiyo inatekeleza kwa vitendo falsafa ya ‘Mpira uchezwe kila Kona na kila Mtaa’ na kwenda sambamba na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amelipa jicho la pekee sekta hiyo ambayo imeanza kuonesha matumaini makubwa baada ya baadhi ya timu za Taifa ikiwemo timu ya wanawake Serengeti Girls kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa.
Mjengwa amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa michezo katika kuhakikisha mpango mkakati wa ushiriki wa Taifa katika mashindano ya kombe la dunia 2030 unafikiwa kwa mafanikio makubwa.
Awali akieleza juu ya Program hiyo, Mkuu wa Program wa KTO Mia Mjengwa Bergdahl alieleza kuwa Program ya Mpira Fursa imeenea nchini kote kupitia vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi na kupitia vyuo hivyo shule za Msingi 86 pia zimenufaika na vijana wanakuza vipaji vyao kuanzia ngazi hiyo ya chini kabisa.
Bi. Mia amesema, wanashirikiana kwa ukaribu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF,) katika kutoa mafunzo kwa makocha ambao wamekuwa wakiwanoa wachezaji katika vyuo na wanategemea kuwa na wachezaji wa mpira wa miguu wanawake kumi elfu kufikia mwaka 2023.
‘’Jitihada zinazofanywa na Serikali zinapaswa kuungwa mkono kwa ukaribu zaidi kupitia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vyuo saba vimepata mafunzo ya kutengeneza mipira kwa kasi hii na ushirikiano baina ya KTO, Serikali, TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara Mama ya Michezo tunategemea timu ya Taifa ya Wanawake itapata wachezaji kutoka vyuo vyetu vya Maendeleo ya Wananchi.’’ Amesema.
Program ya Mpira Fursa imelenga kuwajengea wanawake kujiamini, kucheza mpira wa miguu kwa mlengo wa fursa pamoja na kuondoa mfumo dume na kwa sasa mpira wa miguu utachezwa kila kona na mitaa ili kufikia azma ya kujenga kizazi kinachonufaika na mchezo huo na kuongeza ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano ya kimataifa.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akisaini mmoja ya mpira ambao umetengenezwa katika moja ya vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akikabidhi vifaa vya michezo kwa baadhi ya makocha kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, vifaa hivyo vitavinufaisha vyo pamoja na shule za Msingi 86 zilizofikiwa na program ya Mpira Fursa.
Baadhi ya wadau wakifuatilia ufunguzi huo.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa michezo waliohudhuria ufunguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments