Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Soka Tanzania na mashindano mengine, Klabu mbalimbali nchini zimeendelea kuboresha vikosi vyao kuelekea msimu huo wa 2023-2024.
Habari kubwa zaidi kuelekea msimu ujao wa mashindano, ni panga pangua ya miamba ya soka nchini hususani Klabu za Simba, Yanga na Azam na wengine wengi wanaojiandaa kushiriki msimu huo wa mashindano.
Simba SC imewaacha Wachezaji wao waandamizi, Wachezaji ambao mashabiki wengi wa Soka hawakutarajia kuachwa kwenye Kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Msimbazi - Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Simba SC wameachana na Kiungo wao mkongwe Kikosini hapo, Jonas Gerald Mkude ambaye amedumu Kikosini hapo kwa takribani miaka 13, ikiwa ni tangu apandishwe kutoka Kikosi cha vijana cha timu hiyo msimu wa 2011-2012.
Kiungo mkongwe, Erasto Edward Nyoni (Mzee wa Nyumbii Bombii) naye amepewa mkono wa kwa kheri kwenye Kikosi hicho cha Simba SC baada ya kuhudumu kwa takribani misimu kadhaa tangu aliposajiliwa mwaka 2017 kutoka Azam FC yenye maskani yake Chamazi, Dar es Salaam.
Vile vile, Simba SC imeachana na aliyekuwa Golikipa namba mbili kwenye Kikosi hicho, Beno Kakolanya ambaye alisajiliwa Simba SC mwaka 2019 kutoka Yanga SC.
Beno Kakolanya anakuwa Mchezaji wa tano kuachwa Simba SC baada ya Mlinzi raia wa Ivory Coast, Mohamed Ouattara, na Viungo wa raia wa Nigeria, Nelson Okwa, VÃctor Akpan na Mshambuliaji raia wa Ghana, Augustine Okrah.
Simba pia imeachana na Makocha wake, (Kocha wa Viungo), Kelvin Mandla Ndlomo na Daktari wa timu hiyo, Fareed Cassiem, sanjari na Kocha wa Makipa, Zakaria Chlouha na Kocha wa timu ya Wanawake (Simba Queens), Charles Lukula, raia wa Uganda.
Kwa upande wa Mabingwa wawatezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) Young Africans SC wametangaza kuachana na Mshambuliaji wao mtukutu, raia wa Ghana, Bernard Morrison ambaye alirejea Kikosini hapo mwaka 2022 akitokea Simba SC. Morrison alisajiliwa na Simba SC, usajili uliozua utata kwenye masuala ya mkataba.
Pia, Yanga SC imetangaza kuachana na Mshambuliaji wake raia wa DR Congo, Tuisila Kisinda ambaye alirejea Kikosini hapo msimu wa 2022-2023 akitokea RS Berkane ya Morocco. Kwa mara ya kwanza Kisinda alisajiliwa Yanga SC msimu wa 2020-2021 akitokea AS Vita Club ya nyumbani kwao, DR Congo.
Yanga SC imeachana na Kocha wao wa Mataji, Nasreddine Mohammed Nabi ambaye alitua Kikosini hapo msimu wa 2020-2021 akitokea El Merrikh ya Sudan. Kocha Nabi alipata mafanikio makubwa Yanga SC, aliwafikisha hatua ya Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) na kuwapa mataji mawili ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara na mataji ya Kombe la Shirikisho la ASFC na Ngao ya Jamii.
Hata hivyo, Yanga SC imeachana pia na Mshambuliaji wake, Mtanzania Dickson Ambundo na Kocha wa Magolikipa, raia wa Brazil, Milton Nienov ambaye alitua Kikosini hapo msimu wa 2021-2022 akitokea Simba SC. Nienov alisajiiwa Simba SC msimu wa 2020-2021.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments