Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Wachezaji wa Azam FC waliotajwa kwenye tetesi za kutaka kutimkia katika Klabu za Yanga na Simba, hatimaye wameendelea kubaki katika Kikosi hicho cha matajiri wa Chamazi, Dar es Salaam.
Wachezaji hao ni Kiungo raia wa Ghana, James Akaminko ambaye alitajwa kutaka kusajiliwa na Yanga SC. Uongozi wa Wananchi uliandika barua kwenda Azam FC kutaka huduma ya Kiungo huyo mwenye nguvu, Akaminko sanjari na Mshambuliaji wa timu hiyo, Kipre Junior.
James Akaminko ni rasmi ameongezwa mkataba wa miaka miwili katika Kikosi hicho cha Azam FC, ambapo atakuwa hapo hadi mwaka 2026, mkataba wake utakapoisha rasmi. Akaminko alisajiliwa Azam FC msimu wa 2022-2023 akitokea Great Olimpics ya Ghana.
Azam FC wamembakisha pia Kiungo Mkabaji, Sospeter Bajana ambaye awali tetesi za soka nchini zilimtaja kutaka kusajiliwa na Simba SC. Kiungo huyo wa Kimataifa wa Tanzania, Bajana ameongeza mkataba wa miaka mitatu Kikosini hapo.
Hata hivyo, Azam FC tayari wametangaza kuachana na Wachezaji raia wa Zimbabwe, Bruce Kangwa Amaruce (Mlinzi wa Kushoto), Mshambuliaji Rodgers Kola (Zambia), Kiungo Kenneth Muguna (Kenya), Mshambuliaji Ismail Kader (Tanzania) na Kiungo Mshambuliaji Cleophace Mkandala (Tanzania).
Pia, Azam FC imetangaza kuachana na baadhi ya Wataalamu wa Benchi la Ufundi, Kaimu Kocha Mkuu Kali Ongala, Kocha wa Makipa, Dani Cadena (Hispania) na Mtaalamu wa mazoezi ya viungo (Fitness Coach), Dkt. Moath Hiraoui (Tunisia).
Hadi sasa, Azam FC wametangaza usajili wa Kiungo Mshambuliaji Feisal Salum Feitoto kutoka Young Africans SC.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments