Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) imefuta hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika (2nd Preliminary stage) ambayo ilikuwa inatoa nafasi kwa timu zilizoshindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kucheza hatua hiyo ya mtoano ili kufuzu makundi ya Kombe hilo la Shirikisho.
Kamati hiyo imetoa uamuzi huo na kwamba timu 16 za raundi ya pili ya Michuano yote ya Ligi ya Mabingwa (CAF CL) na Kombe la Shirikisho (CAF CC) zitafuzu hatua ya makundi moja kwa moja kwa timu zilizopata ushindi kwenye raundi hiyo ya pili kanzia msimu ujao wa 2023-2024.
Maana yake, timu inayocheza Ligi ya Mabingwa Afrika endapo itatolewa kwenye hatua ya pili (2nd Preliminary) ya Michuano hiyo haitapata nafasi ya kujiuliza kucheza mtoano (play off) kwenye Kombe la Shirikisho ili kufuzu hatua ya makundi ya Michuano hiyo.
CAF imechukua uamuzi huo katika kikao chake cha Kamati hiyo ya Utendaji kilichofanyika mjini Rabat nchini Morocco. Katika kikao hicho mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo, Michuano mbalimbali inayoratibiwa na Shirikisho hilo, Michuano ya Mataifa ya Afrika na Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika Abidjan nchini Ivory Coast, Julai 13, mwaka huu.
Aidha, Kamati hiyo ya Utendaji imeteua Wajumbe wapya watakaounda Kamati ya Waamuzi wa Shirikisho hilo (CAF); Wajumbe wa Kamati hiyo ya Waamuzi wanaongozwa na Rais Hugues Alain Adjoyi (Benin) na Makamu wa Rais Victor Gomes (Afrika Kusini).
Wajumbe wengine ni Fatou Gaye (Senegal), Dombouya Aboubacar (Guinea), Ali Mohammed Ahmed (Somalia), Tesfanesh Woreta (Ethiopia),
Djamel Haimoudi (Algeria), Hadqa Yahya (Morocco), Olivier Safari Kabene (DR Congo), Louzaya René Daniel (Congo), Inacio Candido (Angola), Gladys Lengwe (Zambia) na Aminu Shantali Shuaibu (Nigeria).
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo imesema inaamini kuwa Kamati hiyo ya Waamuzi itasimamia vizuri Waamuzi hao wakiwemo Waamuzi wa VAR, ‘Match Commisioners’ ili kuhakikisha soka la Afrika linaendelea kufika mbali na kuwa soka la ushindani ulimwenguni kote.
Vile vile, Rais wa Shirikisho hilo, Dkt. Patrice Motsepe ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutembelea makao makuu mapya ya Shirikisho la Soka nchini Morocco yaliyopo mjini Rabat huku akisifia ubora wa makao makuu hayo ambayo yanakidhi viwango vya Kimataifa, Dkt. Motsepe ametoa wito kwa nchi nyingine kuiga mfano wa Morocco.
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF), Wallace Karia (wa tatu kutoka kulia, mstari wa chini) alihudhuria kikao hicho.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments