Dar es Salaam Jumatatu Septemba 2 2024 — Ndondo Cup 2024 imekuwa hadithi ya mafanikio makubwa, ikitumika kama jukwaa lenye nguvu la kutoa huduma za afya na kuimarisha huduma za VVU na chanjo miongoni mwa vijana wa kiume na wanaume nchini Tanzania.
Mpango huu wa kibunifu, unaoongozwa na Serikali ya Marekani kupitia mradi wa Breakthrough ACTION, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), uliweza kuwafikia karibu vijana 10,000 wenye umri wa miaka 15-24 kwa huduma za kinga na upimaji wa VVU na chanjo wakati wa mashindano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam.
Kwa kuwalenga vijana wa kiume wenye umri wa miaka 15-24—kundi ambalo kwa kawaida ni gumu kufikiwa kwa huduma za afya—mradi wa Breakthrough ACTION ulichagua kwa uangalifu Ndondo Cup kama fursa kamili ya kukutana na kundi hili. Kwa Dar es Salaam, mashindano hayo yalivutia zaidi ya watu 70,000, na kati yao, takribani vijana 10,000 walipata huduma za upimaji wa VVU na chanjo, hivyo kugeuza msisimko wa michezo kuwa fursa ya kushiriki katika majadiliano ya afya na kupata huduma za vvu na chanjo kwa hiari. Kwa kuongezea, zaidi ya watu milioni 13 kote nchini walifikiwa kupitia majadiliano katika redio na mitandao ya kijamii yaliyolenga umuhimu wa kinga na upimaji VVU na chanjo.
"Ndondo Cup ni ushahidi wa jinsi michezo inavyoweza kuhamasisha na kuboresha afya ya umma kwa ufanisi," alisema Waziri Nyoni, Mkurugenzi wa Mradi wa Breakthrough ACTION nchini Tanzania. "Ushirikiano wetu na Serikali ya Tanzania na washirika wa wengine wa Serikali ya Marekani, ikiwa ni pamoja na MDH na EpiC, ulikuwa na mchango mkubwa katika kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wanaume na vijana."
Mmoja wa washiriki, aliyejulikana kwa jina Hussein Abdallah, alisema, "Nilikuja kuangalia mechi, lakini niliposikia kuhusu huduma za afya, nikaamua kupima VVU. Mchakato ulikuwa rahisi na ukanifanya nigundue umuhimu wa kujua hali yangu. Pia nilipata chanjo ya COVID-19, ambayo nilikuwa naahirisha kila siku. Mambo yote yamefanyika kiurahisi na bila msongamano."
Ushirikiano huu wa kibunifu wa sekta ya afya na michezo umeweka viwango vipya katika jitihada za kuboresha afya ya umma nchini Tanzania, ukionyesha nguvu ya ushirikishwaji wa jamii katika kufanikisha matokeo chanya ya afya. Ndondo Cup inapoendelea kuhamasisha uelewa wa afya, inaonyesha umuhimu wa ubunifu na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za afya ya umma Tanzania.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments