Ujumbe wa Kevin John na Wachezaji Wengine Serengeti Boys..."Kuweni Makini na Wanyakunyaku wa Bongo"


Kevin John, hili jina limebadilisha hali ya hewa uwanja wa taifa. Mabao 6 michezo 3. Inaonekana yupo siriazi na kazi.

Sijabahatika kuonana nae lakini nikiri tu kwamba ana uwezo.

Pili naweza kutumia waraka huu kuongea na wewe mdogo wangu.

Kwanza nakiri una kipaji lakini pongezi zangu zitakuja nusu nusu. Waswahili husema hifadhi akiba ya maneno.

Kevin upo na rafiki yako Agiri Ngoda nae ana mabao 4.

Nataka niwaambie kwenye soka sisi ni Tanzanjaa na sio Tanzania. Sijui maisha yako yapoje. Labda ndugu umetoka familia njema. Lakini kama umetoka maisha magumu utasumbuliwa sana mdogo wangu. Watakuja na Milion 20 mpaka 40. Utawaona tu. Na wananyenyekea kama mfanyakazi aliyesababisha shoti. Watakuahidi gari, watakuahidi nyumba tena wanaweza kukuahidi kukupeleka ulaya ikiwa wao hawana hata paspoti.

Ukiuangalia mkataba wao utakuwa una uhakika wa chipsi mayai na utakuwa na vijihela vya kuhonga honga watoto wazuri.
Hayo ndio maisha yetu watoto wa mtaani. Tukiona tarakimu nyingi tunachanganyikiwa. Aah hiyo kawaida maisha magumu.

Mdogo wangu kama una roho ndogo utakamatika na tutaishia kukuita fundi. Mitaani huko kila mtu utasikia kevi fundii yule dogo noma sana anajuaa hatari.

Lakini hutokuwa na tofauti na mafundi wa gereji. Unatengeneza bonge la gari unachafuka oili lakini hata baiskeli huna. Si ndio. Ipo hivyo bwana kev.

Wachezaji wetu wa ndani wanacheza mpira mwingi wanazipa timu mapato makubwa na vilabu vinakuwa, mabosi nao akaunti zao zinajaa wewe unatembelea mark II ambayo imepauka rangi na umeshindwa hata kuibadilisha tairi ina kipara. Tena Mark II yenye ulipewa wakati unasaini na hela ya gari bado haijalipwa yote.

Juzi nilikuwa naongelea sakata la umri wa wachezaji. Wapo walionitukana lakini hawakujua namaanisha nini. Mdogo wangu hapa Tanzanjaa vilabu vikubwa hivi vinachotaka ni matokeo. Wapo tayari kuchukua wachezaji wazoefu nje ili tu wawasaidie. Kumbuka wapo wachezaji wengi wenye vipaji hapa bongo wamekwama. Tutasema mara ooh kapigwa msumari, mara kapotezwa na starehe za mademu, mara ooh… Yaani yatasema mengi lakini mwanaharamu wetu ni “UZOEFU”. Hawapewi nafasi ya kutosha. Hawana namba na wako benchi. Sababu kubwa ni vilabu vyetu kuwakumbatia wachezaji wa kigeni ambao huko kwao tayari wameshacheza sana hivyo wana uzoefu. Leo hii Kev tukienda Burkina Faso tunamleta mtu labda anaitwa Keita aliyechezea misimu minne huko kwao tena kacheza mpaka ligi ya mabingwa utashindana nae vipi sasa mdogo wangu? Mtu kashacheza michezo 90 halafu mbaya zaidi watakuja hapa watasema wana miaka 19. Inauma! Ukiuliza utaambiwa nyamaza hatutaki umri wake tunachotaka magoli yake, lakini wanafiki hao hao Taifa stars ikifungwa utasikia ooh hakuna kitu, wachezaji wetu ovuo kabisa, ligi yetu dhaifu n.k n.k n.k. Ligi itakuwa vipi kama sisi tunaifanya dampo?

Hapo ndipo tunapofeli. Ni kweli wana uwezo kwa sababu wana uzoefu huko kwao. Sasa mdogo wangu wewe si umetoka kucheza na vijana wenzio? Utashindana nae namba kweli? Tena mbaya zaidi tuna makocha wa kigeni? Unadhani kocha wa kigeni atakujali ? Yeye ataangalia anayefanya vizuri wewe hatokujali ila kibarua chake kwanza mengine mtajuana wenyewe.

Mdogo wangu wakati wewe ukiwa mdogo na miaka 9 kule Uingereza alikuwepo mwamuzi aliitwa Howard Webb na kocha mmoja anaitwa Sir Alex Ferguson. Huyo mwamuzi alikuwa anaipendelea sana Man United. Wengi walidhani kuwa anaipenda United. La hasha. Haikuwa hivyo. Ila Webb alikuwa Muingereza na alikuwa akiibeba United kwa sababu ilitoa fursa kwa waingereza. Mwisho wa siku uzalendo uliipa United mafanikio. Unapowapa nafasi vijana wadogo katika klabu unahamasisha fursa nyingi zaidi. Kimafanikio.

Lakini hapa kwetu vilabu vyetu havipo tayari kukupa muda wa wewe kupata uzoefu na hawapo tayari kukuvumilia.

Upande wa pili mdogo wangu pia unaweza ukapata nafasi, ukacheza na ukawa staa wa timu kama ilivyo kwa Kichuya. Sawa lakini je unajijua kwamba una uwezo sana kiasi kwamba hupaswi kuendelea kubakia hapa?

Ukicheza hapa Tanzania miaka 5 au 6 utakuwa na miaka 25 au 26 huko. Ukienda Ulaya hawatakupokea kwa umri huo watakuringia sana. Wazungu hawatuamini sana kwenye suala la umri mdogo wangu. Yaani ukienda na miaka 25 wao wanaongeza 10 yaani wanahisi umepunguza 10. Wanatuogopa sana Afrika. Ni ngumu sana kutoka huku kwetu na miaka hiyo na wakakusikiliza.

Unaweza pia ukakosa nafasi ya kwenda kufanya majaribio ulaya. Sawa. Watakapokuja vijana wa Manji, Bakhresa au Mo usikubali kusaini mkataba wa chini ya miaka miwili. Wao wanataka kulinda pesa zao na wewe pia unapaswa kulinda kiwango chako. Ni ngumu sana kuwika msimu wa kwanza wa ligi. Utahitaji muda kidogo. Nasema hivyo maana vilabu vyote vina watu wazoefu kukuzidi. Ukisaini mkataba wa mwaka mmoja ni hatari kwako.

Kwanza kama tunavyojua mwanzo ni mgumu. Wakikuona haujakaa sawa wataenda Burundi au Congo wataleta wahenga wao. Tena mashabiki wao walivyo wanafuki watamoamba huyo mchezaji utadhani kasajiliwa Messi au Ronaldo.

Pia ujue hao wahenga wanajua sana maana tayari ni wazoefu washacheza kabla wewe hujaanza la kwanza lakini wakija utaambiwa unalingana nao umri. Utashangaa mwenyewe unateseka benchi kama Mwambeleko kwa Asante Kwasi. Yatakukuta yale yale ya Dilunga alipotua Yanga. Itabidi ukazunguke kama Dilunga alivyokwenda Ruvu kabla ya Mtibwa na sasa Simba. Tayari hapo ni miaka mitano. Hapo ndipo Simba na Yanga waanze kukumendea tena maana kiwango kishapanda. Ukirudi Simba wanakupa miaka miwili hapo tayari una miaka 25 je ulaya utaenda timu ya nani?

Tunakuhitaji wewe uwe balozi wa soka letu huko nje. Tumeona Faird Musa yupo Hispania sasa ameungana na Chilunda. Hii ni chachu kwa soka letu. Usiogope hata kwenda kucheza Togo wewe nenda. Ukienda kule unajenga jina kama Okwi alivyojenga utawala Msimbazi. Mdogo wangu yupo Mhilu na Mwishiuya wasipokuwa makini nao watazeekea hapa hapa. Ajibu na Feisal salum itabidi wapambane sana kuchukua namba ya Tshishimbi au Makambo.

Nadhani umeona sakata la Mo Ibrahim na Ndemla walivyoteseka kwa Niyonzima.

Hakuna kiongozi wa soka atajali kiwango chako kisha asitazame mfuko wake. Wachache sana wana roho hiyo.

Tanzania tupo nyuma sio kwamba hatuna viwango hapana ila hatuna mipango ya kuwasaidia wachezaji wa ndani. Tunachoabudu ni ubishani wa vijiweni wa mtani wa jadi. Badala tujenge mazingira ya kuwabeba vijana sisi tunakumbatia jipu la makalioni kwa sababu ya aibu.

Nakushauri tafuta vilabu vya nje sio lazima Ulaya. Zunguka kama kaka yako Samatta. Kama utasaini Yanga au Simba au Azam ikifika mahali tafuta fursa kwengine. Usiitegemee VPL sana, ni pagumu mno. Hapa waachie watani na wahenga wao.

Naweza nikawa nimemtumia Kev kama chambo lakini hapa nilikuwa naongea na wadau wote wa soka. Mawakala mameneja makocha na hata vijana wengine wadogo.
Nataka kuwafikishia ujumbe wote ikiwemo serikali kuwasaidia hawa vijana kwenda nje. Sio tu Kev, yupo Morris ambaye hivi majuzi tuliona Anthonio Valencia wa Man United akiposti video yake katika ukurasa wake wa Instagram, wapo akina Nashon, Agiri na wengineo wengi. Najua Kelvin John na wenzake hawawezi kujipeleka wenyewe ulaya lakini TFF itashindwa kujitoa mhanga kwa wachezaji wawili watatu kweli? Serikali kubwa namna hii kweli? Swali langu ni je na kiwango chake nani yupo tayai kumnunulia Kev tiketi ya kwenda kufanya majaribio ulaya n.k? Nimepata fununu kuwa anahitajika na Man United ya England..

Naitwa Privaldinho (Instagram)

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini