Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajiwa kutoa uamuzi utakaotoa mustakabali wa dhamana ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wanaokabiliwa na kesi ya jinai mahakamani hapo leo.
Uamuzi huo unatokana na maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka Novemba 12, uliodai washtakiwa hao wamekiuka masharti ya dhamana kwa kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama na kushindwa kuripoti katika kituo cha Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala.
Upande wa mashtaka ulifikia hatua hiyo baada ya Mbowe kushindwa kufika mahakamani, Novemba Mosi na 8 na Matiko kushindwa kufika Novemba 8, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali wa kesi inayowakabili.
Katika uamuzi huo utakaotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo ndiyo utakaotoa hatima ya wabunge hao wa Hai na Tarime Mjini iwapo wataendelea kubaki uraiani au watatupwa rumande.
Kama Mahakama itaridhika na utetezi wao, itatupilia mbali hoja na mambo ya upande wa mashtaka na hivyo wataendelea kuwa nje kwa dhamana wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa na kusubiri uamuzi.
Lakini kama mahakama hiyo itakubaliana na maombi na hoja za upande wa mashtaka na kutupilia mbali utetezi wao, inaweza ikawafutia dhamana na kuamuru watupwe mahabusu.
Kama mahakama katika uamuzi wake itawafutia dhamana, huo hautakuwa mwisho wao wa kusaka kurejesha haki hiyo ya kuwa huru kwa dhamana.
Washtakiwa wanaweza kuomba tena dhamana kupitia kwa hakimu huyohuyo au kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.
Au wanaweza kuomba tena dhamana lakini hiyo inaweza kuwa na ugumu kufanikiwa kwa sababu Mahakama ina uhuru wa kuwapatia tena dhamana au kuwanyima, kwa kutegemeana na hoja watakazozitoa.
Sponsored by
ZAMOTO MEDIA
0 Comments