Jeshi la Zimbabwe lilitumia "nguvu nyingi" dhidi ya waandamanaji wa upinzani baada ya uchaguzi wa kiti cha Urais.
Hayo yamesemwa na tume maalum iliyoundwa kuchunguza kiini cha ghasia zilizotokea nchini humo.
Watu 6 waliuwawa, baada ya vikosi vya jeshi kutumwa ili kukabiliana na waandamanaji hao waliozua ghasia katika maeneo kadhaa ya mji mkuu Harare mnamo Agosti 1.
Tume huru ya uchunguzi huo, inasema jeshi lilitenda mabaya makubwa bila huruma, wakati ilipoamua kuwamiminia risasi waandamanaji waliokuwa wakitoroka.
Lakini baadhi ya viongozi wa upinzani wanalaumiwa kwa kuchochea ghasia.
Wanajeshi na polisi walikabiliana na waandamanaji ambao walimiminika barabarani, baada ya kuibuka madai kwamba chama tawala cha Zanu-PF, kiliiba kura Julai 30.
"Matokeo ya uchunguzi yanabaini kuwa mauwaji ya watu hao 6, yalitokana na hatua ya jeshi na polisi," sehemu ya ripoti hiyo inasema.
"Matumizi ya risasi yaliyoelekezewa watu, hasa walipokuwa wakitoroka, yanaonyesha bayana kuwa hayakuidhinishwa hasa kutokana na ukubwa wake," inaongeza ripoti hiyo.
Tume hiyo iliyo na wanachama 7 na ambayo iliundwa na Rais Emmerson Mnangagwa, kufuatia ushindi wake finyu wa Urais, ilibaini kuwa kutumwa kwa jeshi kutuliza uhasama huo mjini Harare ulifanywa kwa kufuata sheria.
Mwenyekiti wa tume hiyo ni rais wa zamani wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wa Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange ni miongoni mwa wajumbe wake.
Ripoti hiyo pia imekishutumu chama cha upinzani cha MDC Alliance, kwa kuchochea ghasia, hasa kutokana na hotuba ya baadhi ya viongozi wake.
"Ikiwa maandamano hayo hayangekabiliwa, hali hiyo ingeongezeka na kuwa vigumu kuthibitiwa na hatimaye kuwa mbaya zaidi" inasema.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments