Mkuu Wa Idara Ya Ardhi Kyerwa Apewa Wiki Moja Vinginevyo Kutumbuliwa | ZamotoHabari.

Mkuu Wa Idara Ya Ardhi Kyerwa Apewa Wiki Moja Vinginevyo Kutumbuliwa
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amempa wiki moja Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kuhakikisha anaingiza viwanja 516 katika Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki vinginevyo ataondolewa katika wadhifa huo.

Agizo hilo limafuatia Dkt Mabula kuelezwa na Mkuu huyo wa Idara kuwa katika halmashauri hiyo jumla ya viwanja 348 pekee ndvyo vilivyoingizwa katika Mfumo wa Kielektroniki huku viwanja 516 vikiwa havijaingizwa kwenye mfumo huo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa agizo hilo jana tarehe 15 Machi 2019 wakati akiwa katika mfululizo wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika wilaya za mkoa wa Kagera.

Dkt Mabula alisema kuna uzembe mkubwa kwa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kusimamia uingizaji viwanja kwenye mfumo ambao ndiyo unaosaidia kuongeza mapato ya serikali.

Naibu Waziri alishangazwa na Mkuu huyo wa Idara kushindwa kuingiza idadi hiyo ya viwanja kwenyea mfumo wa kielektroniki katika kipindi cha mwaka mzima wakati alieleza kuwa kwa siku moja anao uwezo wa kuingiza viwanja ishirini.

‘’Kuna uzembe katika kusimamia idara hii ya ardhi na kama mzigo ni mkubwa kwako kusimamia idara hii basi chagua kuachia nafasi moja katia ya Ukuu wa idara ya ardhi au Afisa Ardhi Mteule  ili uweze kuifanyia nafasi moja kwa ufanisi’’ alisema Mabula.

Akigeukia suala la utoaji hati katika halmashauri hiyo ya Kyerwa, Dkt Mabula aliiagiza halmashauri ya Kyerwa kuhakikisha maeneo yote yaliyochukuliwa kwa ajili ya matumizi ya umma yanapatiwa hati ili kuepuka migogoro ya ardhi.

Alisema, migogoro mingi kwenye taasisi za umma inasababishwa na taasisi hizo kutokuwa na hati kwenye maeneo yake na kutolea mfano moja ya maeneo yanayovamiwa sana ni yale ya wazi na kuzitaka  idara husika kusimamia suala hilo kwa makini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashid Mwaimu alisema viwanja vingi katika wilaya yake havina hati jambo alilolieleza kuwa wakati mwingine linawapa ugumu wa kuchukua hatua kwa wamiliki wake ambao aliwaeleza kuwa wengi wameacha maeneo yao kuwa mapori.

Kwa mujibu wa Mwaimu wilaya hiyo imetoa miezi sita kwa wamiliki wote wa viwanja ambao hawajaviendeleza na kuviacha mapori kuviendeleza vinginevyo watafutiwa umiliki wake.

Katika hatua nyingine Dkt Mabula ametaka halamashauri ya wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera kulitumia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wake ili kuondoa uhaba wa makazi kwa watumishi wa halmashauri hiyo.

Alibainisha kuwa, hata kama halmashauri hiyo haihitaji nyumba kwa ajili ya watumishi wake basi inaweza kujengewa nyumba na shirika hilo kwa ajili ya kuutengeneza mji wa Karagwe na wakati huo kuzitumia nyumba hizo kama rasilimali ambapo nyumba hizo zinaweza kupangishwa na  kuiwezesha halmashauri kujipatia kipato.

‘’Halmashauri badala ya kutegemea kuingiza mapato katika baadhi ya vyanzo kama vile kituo cha mabasi wanaweza kulitumia shirika la nyumba kuongeza hadhi ya mji na mapato kwa halmashauri’’ alisema mabula.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini