NA K-VIS BLOG, RUFIJI
UJENZI wa mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya mto Rufiji (RHPP), unaendelea kwa kasi ambapo Kaimu Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu Mhandisi Innocent Luoga amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inautekeleza mradi huo kama ilivyo ahidi.
Mhandisi Luoga ameyasema hayo kwenye eneo la mradi(site) Julai 4, 2019 wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa pamoja na Naibu Waziri wa Nyumba na maendeleo ya Makazi wa Misri, Mhandisi Mahmoud Fahmy Nassar.
Kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na ile ya Elsewedy Electric zote kutoka nchini Misri ndizo zinatekeleza ujenzi wa mradi huo.Mradi wa umeme wa maporomoko ya Mto Rufiji utakuwa na uwezo wa kufua umeme Megawati 2,115.
"Huu ni moja ya miradi mikubwa ambayo Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri Dkt. John Mgufuli inatekeleza na kusimamiwa na wazawa (Watanzania) wenyewe.” Alibainisha Mhandisi Luoga.
Alisema tayari manufaa ya mradi huo yako bayana ambapo watanzania elfu 10,000 wamefaidika na ajira zikiwemo za moja kwa moja kwenye mradi lakini pia za watoa huduma kwa wakandarasi na wajenzi wa mradi huo.
Naye Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Misri Mhandisi Mahmoud Fahmy Nassar alisema mradi wa Rufiji utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa mwezi Juni 2022.
Alisema, Serikali ya Misri imekuwa ikipata taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi na ndiyo maana ameamua kuja kujionea na wao kama Serikali Wameridhika na maendeleo ya utekelezaji wake.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka ambaye naye alikuwepo katika ziara hiyo aliwahakikishia Watanzania kuwa TANESCO imehakikisha eneo hili la mradi linabaki salama kwa maana ya utunzaji wa mazingira.
"Jiografia ya eneo hili ni miamba, eneo ambalo litakuja kujazwa maji kwa ajili ya kufua umeme kingo zake ni miamba na mteremko mkali kwa hiyo kitaalamu sio maeneo ambayo yanakaliwa na Wanyama." Alisema Dkt. Mwinuka.
Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Mhandisi Mahmoud Fahmy Nassar (watatu kushoto), Kaimu Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu Mhandisi Innocent Luoga (wapili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka (wakwanza kushoto), wakiwa na wakandarasi kutoka kampuni za Arab Contractors na Elsewedy za Misri wakiwa eneo la mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya mto Rufiji (RHPP) wa megawati 2, 115 wakati w aziara ya viongozi hao eneo la mradi Julai 4, 2019.
Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Mhandisi Mahmoud Fahmy Nassar (wakwanza kushoto) na Kaimu Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu Mhandisi Innocent Luoga (wapili kushoto), wakimsikiliza mkandarasi kuhusu maendeleo ya mradi.
Ujenzi ukiendelea eneo la mradi
Mashine zikichimbua miamba na majabali huku malori yakipeba mawe.
Dkt. Luoga (mbele) akifuatana na Meneja Miradi wa TANESCO Mhandisi Stephen Manda, (katikati)
Naye Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Misri Mhandisi Mahmoud Fahmy Nassar(wapili kulia) akitembeela eneo la mradi.
Picha ya mshikamano baina ya Tanzania na Misri.
Meneja Miradi TANESCO Mhandisi Stephen Manda (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la mradi (site), kuhusu utekelezaji wa mradi huo Julai 4, 2019.
Picha ya pamoja
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments